Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia idara ya Maendeleo ya Uvuvi imeanzisha operesheni mbili zilizopewa majina ya “Sangawe na Jodari” kwa dhumuni la kuwabana na kuwashughulikia wavuvi haramu wanaochangia kuharibu mazalia ya samaki kwenye mito, mabwawa, maziwa pamoja na maeneo ya ukanda wa bahari ya hindi.
Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo na Uvuvi Magesa Bulayi amesema hayo wakati akiongea na wakazi wa vijiji na wanufaika wa bwawa la Nyumba ya Mungu linalotumiwa na wakazi wa Kilimanjaro na Manyara
Soma Pia Bwawa la Mtera kulindwa
Mkurugenzi huyo amewaonya wavuvi haramu na kusisitiza kuwa kampeni hizo zinalenga kutokomeza uvuvi haramu, huku akitoa siku saba kwa wavuvi haramu wanaotumia nyavu ndogo na makorokocho kuziwasilisha kwa uongozi wa serikali ya Kijiji.
Akielezea namna wavuvi wanavyokiuka sheria za nchi Bulayi amesema kuwa Sheria ya 22 ya mwaka 2003 inawataka wavuvi kufanya uvuvi unaokubalika kisheria ikiwa ni pamoja na kutumia nyavu kubwa katika kuvulia samaki na kuwataka watendaji walio chini yake kuhakikisha wanafanya doria ya mara kwa mara ili kutokomeza uvuvi haramu.
Soma Pia Wavuvi kukopeshwa
Naye Ofisa Uvuvi wilayani Mwanga David Kabodo amedai serikali ya wilaya hiyo imekuwa ikichukua hatua kadhaa kukabiliana na uvuvi haramu ambapo kwa mwaka 2018, wameweza kufanya doria 34 na kufanikiwa kukamata pikipiki 10, ndoo za samaki zipatazo 776 pamoja na kuwafikisha watuhumiwa katika vyombo vya dola ambapo amedai hadi sasa, takribani kesi 53 zimefunguliwa na kati ya hizo, 32 zimemalizwa na watuhumiwa wametakiwa kulipa faini.