Home VIWANDAUZALISHAJI Uzalishaji asali waongezeka Mbinga

Uzalishaji asali waongezeka Mbinga

0 comment 308 views

Uvunaji wa asali katika Halmashauri ya Mji wa Mbinga umeongezeka kwa asilimia 5.1 mwaka 2022/23 ikilinganishwa na mwaka 2021/22.

Akizungumza Novemba 8, 2023 kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Mbinga Amina Seif, Afisa Nyuki wa Halmashauri hiyo Gilbert Gotifrid amesema kuwa katika kipindi hicho tani za asali zilizovunwa ziliongezeka kutoka 3.9 hadi 4.1.

Amebainisha kuwa ongezeko hilo limechagizwa na kuongezeka kwa mwamko wa wananchi katika shughuli za ufugaji wa nyuki.

“Mwamko umekuwa ukiongezeka siku hadi siku ingawa bado si wakuridhisha sana ikilinganishwa na ukubwa wa maeneo ya ufugaji tuliyonayo,” ameeleza.

Gotifrid amesema wafugaji nyuki ambao ni watu binafsi na taasisi wameongezeka kutoka 42 kwa mwaka 2021/2022 hadi kufikia 84 mwaka 2022/23.

Kwa upande mwingine, vikundi vilivyokuwa vinajihusisha na ufugaji wa nyuki viliongezeka kutoka 32 hadi kufikia 40.

Ameeleza kuwa bado fursa za ufugaji nyuki hazijatumiwa ipasavyo.

“Kati ya hekta 900 zilizopo katika milima ya Lipembe ambazo zimetengwa kwa ajili ya shughuli za ufugaji wa nyuki, ni kama asilimia 1.1 tuu zinatumika kwa shughuli hiyo,” amesema.

Gotifrid ameeleza kwamba ili kutumia vizuri fursa zilizopo kitengo chake kimekuwa kikitoa elimu kuhusu ufugaji wa nyuki kupitia vipeperushi pamoja na redio zilizopo katika Halmashauri hiyo.

Akizungumzia umuhimu wa asali amesema mbali na kuwa inawasaidia wafugaji wa nyuki kujipatia pesa na kuongeza kipato chao pia ni muhimu kwa afya.

Upande wa afya amesema asali inafanya uwiano mzuri wa sukari mwilini pia inawasaidia watu wenye vidonda vya tumbo.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter