Naibu Waziri wa Viwanda, na Biashara, Mhandisi Stella Manyanya ameeleza bungeni kuwa hadi Februari mwaka huu, serikali imechukua jumla ya viwanda 14 kutoka kwa wawekezaji ambao wameshindwa kutekeleza mikataba ya mauzo ya viwanda hivyo.
“Kwa sasa viwanda vyote 14 vilivyorejeshwa serikalini vinaandaliwa utaratibu wa kutafuta wawekezaji wenye uwezo wa kuvifufua”. Amesema Mhandisi Manyanya.
Naibu huyo amesema kuwa katika viwanda hivyo, viwanda viwili, Mang’ula Mechanical and Machine Tools na Dakawa Rice Mill Ltd ni kutoka mkoani Morogoro wakati kiwanda cha Morogoro Canvas Mill Ltd kinaendelea kutafutiwa wawekezaji wengine baada ya kufungwa.
Naibu Waziri Manyanya amesema kuwa serikali imelenga kuhakikisha viwanda vyote vilivyofungwa vinaanza kufanya kazi ili kuwasaidia vijana kupata ajira na kuchangia katika uchumi wa nchi huku akiongeza kuwa, kupitia fursa zilizopo hapa nchini, ujenzi wa viwanda vipya ni muhimu.
“Mkoa wa Morogoro una jumla ya viwanda 14 vilivyobinafsishwa kati ya viwanda hivyo, viwanda nane vinafanya kazi na viwanda sita havifanyi kazi”. Ameeleza Naibu huyo.
Aidha, amesema kutokana tathmini waliyofanya, wamegundua kuwa wawekezaji wengi hawatekelezi makubaliano ya mikataba wanayopewa.