Na Mwandishi wetu
Umoja wa Maofisa Watendaji Wakuu wa Kampuni Binafsi (CEOrt) wameandaa kitabu cha “Tanzania’s Industrialisation Journey 2016-2056” ambacho kinaainisha kuwa ukosefu wa vipaumbele, mitaji na mifumo mizuri ya elimu pamoja na umeme wa uhakika vinachangia katika kurudisha nyuma kasi ya nchi yetu kuelekea katika uchumi wa viwanda.
Mwenyekiti wa CEOrt Ali Mufuruki amesema kuwa wameamua kuandika kitabu hicho kama namna mojawapo ya kuunga mkono dhamira ya serikali ya kubadilisha Tanzania kuwa nchi ya viwanda. Ameongeza kuwa ili lengo hilo litimie, ni lazima kuchagua maeneo machache ya kuanzia na kuweka nguvu kubwa ili kuleta maendeleo.
Naye Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango amesema wakati akizindua kitabu hicho kuwa, kitasaidia watunga sera katika sekta ya viwanda kubaini matatizo mbalimbali pamoja na namna ya kuyatatua. Pia kupitia kitabu hicho, sauti ya sekta binafsi itasikika hivyo ni fursa nzuri kwa sekta hiyo kutoa maoni pamoja na ushauri wao kwani itapelekea mafanikio kupatikana kwa haraka zaidi.