Waziri wa Katiba na Sheria Prof. Palamagamba Kabudi amesema endapo mifumo kandamizi inayowaacha nyuma wanawake itaendelea kuwepo, hakuna maendeleo yanayoweza kufikiwa. Prof. Kabudi amesema hayo wakati akifungua tamasha la wanawake na habari (Women in News Summit) jijini Dar es salaam na kuongeza kuwa, wanawake wanayo nafasi kubwa ya kuleta mabadiliko na kutokana na hilo, serikali inathamini na kutambua mchango wao.
Waziri huyo ameeleza kuwa moja ya mipango ya serikali ni kuwawezesha wanawake hasa katika wakati huu ambapo nchi inaelekea kwenye uchumi wa viwanda na amedai kuwa suala hilo limefafanuliwa vizuri katika Mpango wa Taifa wa Maendeleo 2025.
Mbali na kufanya hivyo, imeelezwa kuwa serikali imefanikiwa kuondoa kodi kwenye taulo za kike na kusaidia upatikanaji wake kuwa nafuu, hivyo kuondoa changamoto ya wanafunzi wa kike kutohudhuria shule kwa kukosa taulo hizo. Vilevile, serikali imeandaa utaratibu utakaoruhusu wanawake kupata mikopo kwa kubadili sheria ambazo hapo awali zilikuwa kikwazo kwao.
Prof. Kabudi amesisitiza kuwa endapo vyombo vya habari vitaendelea kuwaonyesha wanawake kama dhaifu na kutowapa nafasi, basi mafanikio yaliyofikiwa yatakosa umuhimu.
“Ili kufikia mafanikio, ni lazima vyombo vya habari viendelee kushirikiana na serikali ili sauti za wanawake zisikike katika muundo unaofaa, usiowadhalilisha utu wao, bali wanayoyafanya na kuwaonyesha kama mashujaa wa mabadiliko”. Amesema Waziri Kabudi.