Wanawake wajasiriamali kutoka kijiji cha Mswakini kilichopo wilaya ya Monduli wamezindua kiwanda chao cha kuchakata ngozi kwa kupata ufadhili kupitia Shirika la OIKOS kwa lengo la kujijenga kiuchumi, kujitengenezea ajira kupitia ngozi pamoja na kuunga mkono juhudi za serikali kuelekea Tanzania ya viwanda.
Akizungumza katika hafla hiyo iliyoambatana na utoaji wa vyeti kwa wajasiriamali waliofuzu mafunzo ya uchakataji, Mkuu wa wilaya ya Monduli Idd Hassan Kimanta aliyekuwa mgeni rasmi, amewapongeza akina mama hao kwa uamuzi huo na kuwaahidi kupitia halmashauri ya wilaya ya Monduli atahakikisha wanapata mkopo ili kuongeza mtaji.
Kimanta pia amelishukuru shirika la Misaada la Marekani (USAID) kwa kulipatia fedha Shirika la OIKOS linalojishughulisha na ulinzi wa viumbe hai na matumizi endelevu ya rasilimali za asili, ambalo ndilo lililosimamia mchakato wote kupitia mradi wa Ikolojia Hatarini kaskazini mwa Tanzania, ikiwa ni matokeo ya wanawake hao kujiunga pamoja ili kupata ufadhili huo.
Baadhi ya wadau waliokuwepo katika hafla hiyo wamezungumzia ujio wa kiwanda hicho na kusema kitafungua fursa nyingi kwa wakazi wa eneo hilo pamoja na jamii zinazojishughulisha na ufugaji.