Na Mwandishi wetu
Muungano wa Ulaya umetoa ufadhili wa Euro milioni 1400 ambazo ni sawa na Sh 3.7 Bilioni za kitanzania ili kusaidia miradi minne nchini ikiwemo kupitia upya sera ya viwanda. Msaada huo umekuwa kama ishara ya kuunga mkono mpango wa serikali wa kuingia uchumi wa kati kupitia viwanda.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam jana, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Charles Mwijage amesema fedha hizo zitatumika kuwezesha mnyororo wa thamani wa alizeti hasa kuimarisha viwango na ubora. Pia zitasaidia mnyororo wa thamani na kuongeza thamani kwenye mazao ya kilimo pamoja na yale yasiyo ya kilimo.
Mwijage pia amezungumzia suala la viwanda vilivyobinafsishwa, ambapo amedai kati ya viwanda 156 ni viwanda 62 tu vinavyofanya kazi kikamilifu. Waziri huyo ameongeza kuwa bado taarifa zinaendelea kupokelewa na timu iliyopo Dodoma.
Amesema serikali haikusudii kutaifisha kiwanda chochote. Hivyo amewataka ambao wameshindwa kuendeleza viwanda hivyo kuvirejesha serikalini ili wale wenye uwezo wa kufanya hivyo wapewe nafasi hiyo.