Home KILIMOKILIMO BIASHARA Mnada wa kwanza wa chai utawanufaisha wakulima Tanzania?

Mnada wa kwanza wa chai utawanufaisha wakulima Tanzania?

0 comment 212 views

Novemba 13, 2023, Bodi ya Chai Tanzania (TBT) iliweka historia kufuatia uzinduzi wa Mnada wa kwanza wa Kimataifa wa Chai.

Mnada huo, unaolenga kuongeza thamani kwenye zao la chai nchini ili kuwa sehemu ya mchango katika Pato la Taifa. Mnada huo utakakuwa unaendeshwa na Soko la Bidhaa Tanzania (TMX).

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Dkt. Hussein Mohamed Omar ndiye alikuwa mgeni rasmi katika mnada huo akimwakilisha Katibu Mkuu Gerald Mweli na kuhudhuriwa na Mkurugenzi Mkuu wa TBT Mary Kipeja, Mwenyekiti wa Bodi ya Chai Hamis Umande, na Mwenyekiti wa TMX Charles Singili uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Dkt. Omar amepongeza hatua ya kuanzishwa kwa Mnada huo huku akibainisha kuwa ni matokeo ya mkakati kabambe wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan unaolenga kuongeza thamani kwenye mazao nchini ili yachangie kikamilifu katika Pato la Taifa.

“Ili kuhakikisha azma hiyo inatimia, TBT ihakikishe kuwa inatekeleza wajibu wake kwa ufanisi na kuchochea mashirikiano mazuri na nchi jirani inayozalisha zao la chai kwa kuhamasisha matumizi ya mnada wa Tanzania.

Endeleeni kushirikisha sekta binafsi katika maendeleo ya zao la chai, wekeni mikakati ya kuongeza uzalishaji wa zao la chai na kuimarisha ubora wake kwa kuanzisha mashamba mapya na kujenga viwanda vya chai nchini,” amesema Dkt. Omar.

Ameongeza kuwa Bodi ya Chai iweke bei nzuri ya chai ili kuvutia zaidi ushiriki wa wananchi kwenye zao hilo na kuhakikisha viwanda vya chai vinawalipa kwa wakati wakulima ili kuwahamasisha kulima kwa wingi.

Mkurugenzi Mkuu wa TBT Mary Kipeja

Mkurugenzi wa TBT Mary Kipeja anabaisha kuwa hapo awali mnada huo ulikuwa ukifanyika Mombasa nchini Kenya.

Anaeleza kuwa ni asilimia 15 pekee ya chai inayolimwa Tanzania huuzwa ndani ya nchini huku asilimia 85 ikisafirishwa nje ya nchi kupitia mnada wa chai Mombasa pamoja na mauzo ya moja kwa moja.

“Mnada huu wa kwanza nchini unalenga kuongeza thamani ya zao la chai, kutafuta masoko, na kuuza bidhaa za chai,” amesema Kipeja.

Anabainisha kuwa, kutokana na Tanzania kushiriki katika mnada wa chai Mombasa, imekuwa ikikumbana na changamoto kadhaa ikiwemo umbali wa kutoka kwenye mashamba ya chai hapa nchini hadi kufika kwenye mnada huo nchini Kenya.

“Hatua hiyo itapunguza gharama za kimasoko za wasindikaji ikiwemo gharama ya kusafirisha chai hadi Mombasa itapungua kwa asilimia 50 hali itakayoleta unafuu kwa wakulima nchini,” ameeleza Kipeja.

Kwa upande wa usafirishaji amesema bandari za Dar es Salaam na ile ya Tanga zitatumika kusafirisha chai itakayouzwa kwenye mnada, hivyo serikali itapata mapato na ajira kwa Watanzania zitaongeka.

Anaeleza kuwa “kwa kuwa mnada sasa utakuwa ukisimmaiwa na kuendeshwa hapa nchini, uwazi wa bei ya chai utaongezeka kwa kiasi kikubwa na kuongeza uzalishaji.

Akizungumzia swala la uhifadhi na usindikaji Kipeja ameeleza kuwa “Serikali imeweza kulipia gharama zote za usindikaji wa chai kwenye ghala letu, hivyo wakulima wakileta chai kwenye ghala hawatalipa gharama za uhifadhi, natoa wito tulitumie ghala hili ili liweze kujaa, mlikuwa mmezoea mnalipa gharama lakini sasa ni bure”.

Ameeleza kuwa pato la wakulima wakubwa na wadogo linatarajiwa kubadilika kwa kuwa fedha zilizokuwa zikitumika kusafirisha mazao kwa umbali mrefu ili kufika sokoni zitatumika kuimarisha mashamba yao.

Aina za chai zinazopatikana Tanzania ni pamoja na CTC Black Tea, Orthodox Black Tea, Orthodox Green Tea, Infusion Tea na Herbal Tea.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter