Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya utumishi wa umma Dk. Laurean Ndumbaro amesema Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China imetoa fursa 659 za mafunzo ambapo takribani watumishi wa umma 4,812 watanufaika na mafunzo hayo.
Dk. Ndumbaro ameeleza kuwa mafunzo hayo yanatoa kipaumbele kwa sekta zilizopo katika mpango wa maendeleo wa taifa kwa miaka mitano (2017-2021) zikiwa ni pamoja na Tehama, uhandisi wa viwanda, kilimo, elimu, uchumi, biashara, afya pamoja na utawala bora.
Mtendaji huyo amewataka watumishi wote wa umma kuchangamkia fursa hii kwani mafunzo haya yatawasaidia katika utendaji wao wa kazi na kuwawezesha kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi. Vilevile, ameelekeza waajiri kuwawezesha watumishi walio chini yao kuwa miongoni mwa watakaohudhuria mafunzo haya kwani ni haki yao kwa mujibu wa sheria.