Home BENKI Taasisi za fedha zinapoteza fursa vijijini

Taasisi za fedha zinapoteza fursa vijijini

0 comment 106 views

Huduma za kifedha ni moja katika nguzo muhimu kwa ajili ya maendeleo ya wananchi pamoja na taifa kwa ujumla. Kupitia huduma hizi watu wanapatiwa fursa ya kutunza fedha zao kwa usalama zaidi, kufahamu zaidi kuhusu masuala ya akiba na vilevile kupitia huduma rasmi za kifedha upatikanaji wa mikopo kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kimaendeleo unakuwa rahisi. Japokuwa taasisi za kifedha zina umuhimu mkubwa kwa jamii nzima, zinapatikana kwa urahisi zaidi mijini kuliko vijijini. Wengi huimarisha huduma zao sehemu hizi na kuwaweka kando wale waishiyo kijijini.

Ukilinganisha upatikanaji wa huduma hizi kati ya vijijini na mijini, ukweli ni kwamba kuna utofauti mkubwa sana. Japokuwa huduma hizi zinapatikana vijijini, mara nyingi zinakuwa mbali na wengi wanaohitaji huduma hizo hivyo asilimia kubwa ya waishio vijijini huona ni usumbufu kutumia muda mrefu na gharama kubwa ya usafiri kufuata huduma za kifedha zilipo, hali inayopelekea wengi kuendelea kuhifadhi fedha zao katika mifumo isiyo rasmi na kuendelea kutokuwa na elimu ya kutosha kuhusu umuhimu wa taasisi hizo.

Pia changamoto nyingine inayopelekea huduma za kifedha kufanya kazi kwa uchache katika sehemu za vijijini ni uelewa mdogo wa wakazi wa jamii hizo kuhusiana na mifumo rasmi ya kutunza fedha. Tofauti na mijini, ni watu wachache mno vijijini ndio wana elimu ya umuhimu wa benki pamoja na taasisi nyingine za kifedha na hivyo watu wengi huachwa nyuma katika masuala haya. Ni jukumu la serikali, taasisi binafsi pamoja na wadau wote wa maendeleo kutoa elimu kuhusiana na huduma za kifedha ili kubadili mitazamo waliyonayo wakazi wengi wa vijijini.

Kutokuwepo kwa mashirika ya kutosha kwa ajili ya kutoa huduma za kifedha vijijini inawarudisha nyuma watu hawa kwa kiasi kikubwa. Bila uwepo wao wakazi wa maeneo haya wanakosa fursa ya kupata huduma muhimu ambazo ni nguzo katika maendeleo yao. Hii pia inawaathiri kiuchumi kwasababu wanakosa nafasi ya kuomba mikopo pale wanapohitaji kuendeleza shughuli zao mbalimbali za kimaendeleo ndio maana wengi hukwama na kubakia tu kuwa wafanyabiashara wadogo.

Katika kasi nchi yetu iliyonayo hivi sasa katika kuboresha sekta mbalimbali za maendeleo, ni vizuri kama waishio pembezoni mwa miji mikubwa nao wakapewa nafasi sawa za kifedha kama ilivyo kwa wengine. Ni vizuri Tanzania yote ikawa na huduma bora za kifedha na ili lengo hilo litimie kuna sababu kubwa ya elimu zaidi kuhusiana na umuhimu wa hudumza hizi kutolewa vijijini ili kuwafikia watu wengi zaidi.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter