Home BIASHARA Hatua zinazochukuliwa kudhibiti mfumuko wa bei

Hatua zinazochukuliwa kudhibiti mfumuko wa bei

0 comment 120 views

Mfumuko wa bei ni neno ambalo sio geni katika masikio ya walio wengi kwani ni hali ambayo imekuwa ikizikumba jamii mbalimbali duniani ikiwa ni matokeo ya kuongezeka kwa bei ya bidhaa au huduma kutokana na kupatikana kwake kwa uhaba au nadra sana. Mfumuko wa bei unaweza kufasiriwa kama kiwango ambacho bei zinaongezeka zaidi kwa muda, na kusababisha kushuka kwa thamani ya ununuzi wa pesa.

Zipo sababu nyingi zinazoweza kusababisha mfumuko wa bei, zikiwemo upandaji wa bei za bidhaa zinazoagizwa toka nje , vita, uhaba wa chakula unaotokana na uzalishaji mdogo nchini. Mfumuko wa bei unakuwepo hasa tu pale ambapo ujazi wa fedha unaongezeka kwa kasi kuliko uzalishaji wa bidhaa na huduma.

Tanzania ni moja kati ya nchi zinazokumbwa na mfumuko wa bei mara kwa mara. Hizi ni sababu zinazopelekea hali hiyo.

  1. Upungufu mkubwa wa chakula katika kanda ya Afrika Mashariki ambao mara nyingi unatokana na ukame katika mataifa jirani ikiwa ni pamoja na Somalia, Ethiopia, Sudan, Uganda na kaskazini mwa Kenya. Hali ambayo imekuwa ikipelekea kupanda kwa nafaka hasa mahindi na mchele.
  2. Kupungua kwa uzalishaji wa nafaka hususan katika maeneo yanayozalisha mahindi na mpunga nchini.
  3. Kupanda kwa bidhaa za Petroli katika soko la dunia. Hali hii inapelekea ongezeko la gharama za usafirishaji ikiambatana na kuongezeka kwa gharama za vipuri vya magari,sambamba na usafirishaji wa bidhaa mbalimbali kutoka sehemu moja kwenda nyingine.

Serikali ya Tanzania imekuwa ikichukua hatua kadhaa katika kupambana na mfumuko wa bei na kuhakikisha wananchi wanapata huduma na bidhaa katika hali inayorodhisha. hatua hizo ni pamoja na:

  1. Serikali imekuwa ikitoa mgawanyo mzuri wa vyakula unaoendana na mahitaji ya wananchi kwa kununua mazao ya chakula kutoka kwa Wakala wa Chakula wa Serikali (NFRA) na kuuza akiba kwa bei nafuu ili kuweza kupunguza kasi ya ongezeko la bei ya mazao hasa mahindi.
  2. Kuanzisha sera mbalimbali zinazohamasisha uzalishaji kwa wingi- Serikali ya Tanzania imekuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha wananchi kuzalisha bidhaa za mazao kwa wingi ili kuhakikisha nchi inakuwa na chakula cha kutosha katika  nyakati tofauti tofauti. Baadhi ya Sera hizo ni pamoja na ‘Kilimo Kwanza’ sera ambayo imekuwa ikiambatana na utoaji wa Mbolea za Ruzuku pamoja na ‘Shamba Darasa’ kwa wakulima, mambo ambayo kwa kiasi yameweza kufanikisha upatikanaji wa chakula. Pia Serikali imeweza kutoa msamaha wa kodi kwenye vyakula vinavyoagizwa kutoka nje ya nvhi ikiwa ni moja ya jitihada za kupunguza makali ya mfumuko wa bei nchini Tanzania.
  3. Serikali kuiongezea Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) uwezo wa kudhibiti ongezeko holela la bei za mafuta pamoja na kusimamia mwenendo ,upatikanaji, usambazaji na uuzaji wa mafuta nchini Tanzania.
  4. Kuboresha miundombinu ili kurahisisha usambazaji wa zana na mazao ya kilimo pamoja na bidhaa nyingine ili kupunguza gharama za usafirshaji ambazo zinachangia kuwepo kwa mfumuko wa bei nchini Tanzania.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter