Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo nchini (SIDO) Prof. Sylvester Mpanduji amesema shirika hilo limejipanga kutoa mafunzo maalum kwa wajasiriamali wadogo ili kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika kujenga uchumi wa kati na wa viwanda ifikapo mwaka 2025.
Prof. Mpanduji ameeleza kuwa shirika hilo lipo imara na bado linaendesha zoezi la kutoa mafunzo kwa wajasiriamali kote nchini. Mkurugenzi huyo amesema shirika hilo linaunga mkono azma ya serikali ya kufanya Tanzania kuwa nchi yenye uchumi wa viwanda na wamekuwa wakihamasisha watanzania kuwa wawekezaji katika viwanda vidogo ambavyo havina gharama kubwa sana ili kuvijengea uwezo na kuvikuza hadi kufikia kuwa viwanda vya kati au vikubwa.
Mkurugenzi huyo amesema jukumu kubwa la shirika hilo ni kuhamasisha na kuthaminisha viwanda vidogo ambavyo vina uwezo kwa kuajiri watu zaidi ya watano huku gharama ya uendeshaji ikiwa kati ya milioni 10 na 15.