Home BIASHARA Vivutio vinavyoing’arisha Tanzania kimataifa

Vivutio vinavyoing’arisha Tanzania kimataifa

0 comment 66 views

Moja kati ya vitu vinavyoitambulisha vyema Tanzania katika sekta ya utalii ni pamoja na uwepo wa Mlima Kilimanjaro, mlima wa kwanza kwa urefu barani Afrika na wa tatu duniani, mbuga na hifadhi zenye kuvutia na zenye upekee wa aina yake kama vile Serengeti, Ngorongoro, Manyara, Mikumi, Udzungwa, Katavi, Ruaha, na nyinginezo zikiwa ni baadhi tu kati ya vivutio vingi  vinavyoiweka Tanzania juu katika suala zima la utalii.

Majengo na miji ya kihistoria pamoja na mapango hauwezi kuvitenganisha vitu hivi katika sekta hii. Zanzibar meitajwa kuwa sehemu iliyobarikiwa kuwa na fukwe nzuri na za kuvutia bado ina vitu vingi na vizuri ikiwemo mji mkongwe wa Zanzibar unaobebwa na historia ya uwepo wa ngome kongwe, tamaduni pamoja na uwepo wa marashi ya pemba yenye kunukia ni vitu vinavyowavutia watalii wengi kutembelea.

Miaka ya hivi karibuni imeshuhudiwa watu maarufu duniani wakiwemo wasanii wakubwa, wacheza mpira, marais wa nchi mbalimbali na wastaafu wakizuru nchini na kutembelea vivutio hivyo huku wakiahidi kuendelea kuitangaza zaidi  Tanzania katika soko la utalii duniani.

Ripoti iliyotolewa na Wizara ya Maliasili na Utalii Mei 03 mwaka huu imeonyesha sekta hiyo kukua zaidi kutokana na ongezeko la watalii  na kufikia watu Milioni 1.3 ikilinganishwa na idadi ya Mil 1.2 kwa mwaka 2016, raia wa Marekani wakiongoza kwa kutembelea akiwemo Rais Mstaafu wa Marekani Barack Obama.

Wastani wa pato lililotokana na utalii ulitajwa kuongezeka kutoka Dola za Kimarekani Milioni 2.1 kwa mwaka 2016 hadi kufikia Dola Milioni 2.2 kwa mwaka 2017.

Zipo sababu mbalimbali zinazowavutia watalii kuendelea kuitembelea Tanzania ukilinganisha na nchi nyingine za Afrika Mashariki.

Uwepo wa miundombinu bora

Serikali ya Tanzania imekuwa ikijitahidi katika kuboresha miundombinu katika sehemu za utalii ikiwa ni pamoja na uwepo wa magari ya utalii, uboreshaji na ujenzi wa barabara kwa kiwango cha rami kutoka sehemu moja ya utalii hadi nyingine, uimarishaji wa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) pia sambamba na maboresho ya viwanja vya ndege ni moja ya sababu zinzopelekea ongezeko la watalii nchini.

Uimarishaji wa ulinzi na usalama

Moja ya vitu vinavyovutia watalii ni uwepo wa amani na utulivu katika nchi ya Tanzania. Hii inatokana na uimarishwaji wa ulinzi na usalama vikiambatana na uungwana waliojijengea watanzania. Serikali pia imekuwa ikiimarisha usalama wa vivutio hivyo ili viendelee kuwepo na kulinufaisha taifa. Hivi karibuni serikali ilitangaza kuweka kamera za usalama katika mbuga ya mikumi ikiwa ni sehemu ya kuhakikisha wanyama wanalindwa.

Matukio ya kihistoria na kitamaduni

Shughuli nyingi za utalii hasa katika maeneo ya kaskazini mwa Tanzania yamekuwa yakiambatana na maonyesho ya matukio ya kiutamaduni yanayofanywa kwa kiasi kikubwa na kabila la wamasai. Watalii wengi wamekuwa wakivutiwa kuja Tanzania hasa sehemu za kaskazini kutokana na michezo ya kimaasai ikiwemo mchezo wa kupandisha mori ambao ni maarufu sana. Wachonga vinyago nao ni moja kati ya vivutio vikubwa vya utalii.

Mazingira mazuri ya starehe na mapumziko

Moja ya vitu vinavyowafanya watu wengi kutalii ni pamoja na kutaka kupumzika na kupunguza msongamano wa shughuli, kustarehe na kujipumzisha. Hivyo watalii wanahitaji kupata sehemu tulivu, safi na yenye kuvutia. Kampuni binafsi pamoja na serikali zimekuwa zikiwekeza katika ujenzi wa hoteli nzuri na zenye ubora wa kiwango cha kimataifa, kuweka mazingira katika hali ya usafi na yenye kuvutia.Uwepo wa sehemu za mazoezi ni moja ya vitu vinavyowavutia watalii.

Hali ya hewa

Vivutio vingi vilivyopo Tanzania vipo katika mazingira rafiki yanayoendana na mabadiliko ya misimu yote ya mwaka mzima. Hivyo uwepo wa watalii katika sehemu za vivutio umekuwa ni wa kila siku. Kutokuwepo kwa majanga ya asili kama jangwa, mafuriko, tetemeko, milipuko wa volcano katika sehemu za vivutio hivyo ni moja kati ya vitu vinavyowafanya kujihakikishia usalama.

Msukumo wa serikali

Kutokana na ukweli usiopingika kuwa sekta ya utalii ni moja ya sekta kubwa zinazoliingizia taifa pesa nyingi. Serikali imekuwa ikitilia mkazo katika kuboresha sekta hii ikiwa ni kutenga na kuongeza mapori ya hifadhi za akiba, kulinda maliasili zilizo katika hatari ya kutoweka kama vile vichaka virefu mkoani Singida, ni matokeo ya serikali kuona umuhimu wa sekta hii nyeti.

 

 

Tanzania ni sehemu salama kwa utalii na yenye kila kitu cha kuvutia. Tuzilinde maliasili zetu ili zije zinufaishe pia vizazi vya miaka ijayo.

 

 

 

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter