Home FEDHA Jinsi pombe inavyochochea umaskini

Jinsi pombe inavyochochea umaskini

0 comment 112 views

Pombe imekuwa changamoto katika kufikia malengo sio tu hapa nchini bali duniani kote kwa ujumla. Vijana ambao ndio nguvu kazi ya taifa wameathirika na matumizi ya pombe kupita kiasi. Unywaji wa pombe uliokithiri umekuwa chanzo cha watu wengi sio tu vijana kuendelea kuwepo katika dimbwi la umaskini kwa sababu wamekuwa watumwa wa ulevi na wanaona maisha yao hayawezi kusonga bila pombe. Inapaswa kujiuliza, tutaweza kufikia nchi yenye uchumi wa kati kama tutaendelea kushuhudia pombe ikiteketeza nguvu kazi ya taifa bila kuchukua hatua yoyote?

Kundi kubwa la vijana huanza kujihusisha na ulevi wakiwa wadogo hivyo wanapata wakati mgumu kuacha mazoea haya kadri miaka inavyosonga. Tabia hii inachangiwa kwa kiasi kikubwa na watoto kukosa malezi mazuri kutoka kwa wazazi na familia na vile vile ushawishi kutoka kwa marafiki zao wa karibu. Ni kweli kuwa huwezi kuingilia maamuzi binafsi ya mtu na kumpiga marufuku kutumia kilevi endapo anatumia gharama zake mwenyewe. Lakini unywaji wa pombe uliokithiri haumuumizi mtu mmoja tu bali hata wale wa karibu yake na jamii kwa ujumla.

Kwa haraka tu tujiulize, mlevi ni mtu wa kuweka akiba? Ni mtu mwenye kutumia fedha zake kistaarabu? Ni mtunzaji wa familia? Hapana. Watu hawa hutafuta fedha na kuzimaliza zote sehemu za starehe. Hivyo maamuzi yao hayawaathiri wao tu bali hata wale ambao wanawategemea. Kama watoto watashindwa kupelekwa shuleni watakuwa na maisha gani kesho? Kama kila shilingi inayoingizwa inatumika kugharamia pombe, watoto hawa wataishi vipi kama hawajawekewa misingi imara na wale wanaowategemea?

Unywaji pombe umekuwa sababu mojawapo ya watu wa hali ya chini kuendelea kuwa chini kutokana na kwamba, wanashindwa kutimiza mahitaji mengine muhimu au hata kuwekeza katika biashara sababu wanakosa muongozo wa namna na kutumia kile wanachopata. Matokeo yake, watu hawa wanashindwa kupambana na umaskini na hivyo wanabakia katika hali hiyo

Ulevi pia umekuwa chanzo cha migogoro katika familia na jamii kwa ujumla. Tumeshuhudia familia zikiiingia katika migogoro kutokana na hili. Mbali na kwamba migogoro hii mara nyingi huishia kuwaumiza zaidi watoto, familia kusambaratika na kukosa msaada waliokuwa wanaupata mwanzo kunaweza kuwaweka katika nafasi mbaya kiuchumi. Hivyo jambo hili sio la kufumbiwa macho. Ni lazima watu wenye matatizo ya kunywa kupita kiasi wasaidiwe. Starehe hii ikipitiliza, inawaumiza wengine.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter