Nchi za Afrika Mashariki zimetajwa kuwa miongoni mwa nchi zenye rasilimali nyingi zenye uwezo wa kuzalisha nishati lakini zimeshindwa kulifanikisha hilo na hivyo kurudisha nyuma sekta ya viwanda katika ukanda huo. Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) anayejishughulisha na uzalishaji na huduma za jamii Christopher Bazivamo kwenye maonyesho ya uzalishaji nishati jijini Arusha.
Katibu huyo amedai kuwa licha ya kuwepo rasilimali nyingi katika ukanda wa Afrika Mashariki bado hazijatumika ipasavyo kuongeza kiwango cha nishati kinachohitajika.
“Ninapenda kuishukuru serikali ya Ujerumani kwa kushirikiana na EAC kuhamasisha matumizi ya nishati jadidifu katika eneo hili lenye nchi sita, likiwa limebarikiwa vyanzo vya kutosha vya kuzalisha nishati hiyo kutumia kutumia fursa hiyo ikizingatiwa malengo yake ni kuwa jumuiya imara kiuchumi” Alisema Bazimavo.
Aidha ameongeza kuwa kuna haja kubwa ya Jumuiya kuboresha na kuongeza uzalishaji wa nishati jadidifu kutokana na idadi kubwa ya wananchi kuishi vijijini huku wakitegemea nishati duni kama vile kuni, mkaa, mabaki ya mazao shambani baada ya mavuno.
Naye Mratibu wa Shirika la Maendeleo ya Kimataifa ya Ujerumani (GIZ), Dk Kirsten Focken alisema nchi ya Ujerumani imekuwa ikitumia nishati jadidifu kwa zaidi ya miaka 30 na imeleta matokeo mazuri na hivyo kuzishauri nchi wanajumuiya wa Afrika Mashariki kutumia nishati hiyo kwa ajili ya maendeleo ya viwanda.