Home BENKI TADB yafufua viwanda Kagera

TADB yafufua viwanda Kagera

0 comment 186 views

Mkuu wa wilaya ya Karagwe Godfrey Mheruka amesema mkopo uliotolewa na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kwa lengo la kuinua sekta ya kilimo kupitia zao la kahawa mkoani Kagera, umechangia kufufua viwanda na kutengeneza ajira za wanawake wilayani humo. Mheruka ameongeza kuwa wilaya ya Karagwe ina jumla ya viwanda vitano vya kukoboa kahawa ambapo kwa sasa, kila kiwanda kina wanawake zaidi ya 400.

“Tangu mkopo utolewe na benki ya kilimo, kasi ya ukusanyaji wa kahawa katika msimu wa mwaka 2018/2019 umeweza kuleta manufaa makubwa kwa wananchi wilaya hapa. Zaidi ya wanawake 2,000 wamepata ajira za kufanya kazi za upembuaji kahawa ili kuongeza thamani katika soko la kimataifa”. Ameeleza Mheruka.

Katika maelezo yake, Mheruka amesema tangu TADB itoe mkopo kuinua zao la kahawa mkoani Kagera, kasi ya ukusanyaji imeongezeka huku mzunguko wa fedha kwa wakulima nao ukiwa wa kuridhisha. Mheruka amedai mfumo mpya wa serikali na benki hiyo umeleta mafanikio makubwa kwa upande wa uzalishaji na kuinua maisha ya wakulima kwa ujumla.

“Baada ya kahawa kukobolewa kiwandani, wanawake ndio wanaochambua punje bora na zile ambazo si nzuri, kila kiwanda kina wanawake wasio chini ya 400, hii ndiyo dhana ya Rais John Magufuli anayotaka Tanzania ya viwanda itakayozalisha ajira kwa watanzania”. Amesisitiza Mkuu huyo wa wilaya.

Kwa upande wao, baadhi ya wamiliki wa viwanda vya kukoboa kahawa wamekiri ongezeko la makusanyo ya kahawa wakisema mkopo uliotolewa na TADB umesaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza uzalishaji.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter