Home BIASHARA Biashara ya asali: Fursa isiyokimbiliwa na wengi

Biashara ya asali: Fursa isiyokimbiliwa na wengi

0 comment 278 views

Mpaka sasa Tanzania na Ethiopia ndio nchi pekee zinazoongoza kwa uzalishaji wa asali duniani huku uhitaji ukiwa mkubwa zaidi ukilinganisha na uzalishaji wake. Novemba 2016 maonyesho ya asali yalifanyika hapa nchini yakihusisha wajasiriamali wanaojishughulisha na ufugaji wa nyuki na wazalishaji wa asali, wadau mbalimbali pamoja na wataalamu wa masuala ya ufugaji nyuki fursa iliyowapa wajasiriamali hao kufahamu uhitaji wa soko na mbinu bora za kupata soko.

Akizungumza katika maonyesho hayo, Katibu wa baraza la  asali Tanzania Dk. Kansatan Kabialo alisema jumla ya tani 9,380 za asali zimekuwa zikizalishwa kila mwaka sawa na asilimia 7 tu ya uzalishaji nchini huku nta zikifikia tani 625.3 zilizoingiza kiasi cha Sh. 14 bilioni.

“Kwa kweli tunazalisha kiasi kidogo sana ndio maana tumeandaa maonyesho haya ili tukutane na wadau mbalimbali wa asali na kuhamasisha wafugaji wafuge zaidi”. Alisema Katibu huyo.

Kwa mujibu wa Dk. Kabialo biashara hii imeweza kuajiri watu takribani milioni mbili na kuendelea nchini kote huku idadi hiyo ikihusisha warinaji, wafunga vifungashio, wafugaji, na watengeneza mizinga. Asali ni moja ya bidhaa zinazompa muuzaji faida kubwa endapo tu ataamua kuwekeza kuanzia ufugaji hadi urinaji. Kwa wastani lita moja ya asali huuzwa shilingi 10,000 huku mikoa ya Tabora, Kigoma, Dodoma, na Singida ikifuatiwa na Tanga, Katavi, Iringa, Kilimanjaro na Arusha ikiongoza kwa uzalishaji nchini.

Akizungumza kwenye maonyesho hayo, Dk. Kabialo alisisitiza kuwa asali haiharibiki kwa muda mrefu kama yalivyo mazao mengine ya chakula, kwani ina uwezo wa kukaa zaidi ya miaka 30 na kudai kuwa, hubadilika rangi na kuwa nyeusi, na ndio sababu kuu ya Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) kutowalazimisha wajasiriamali wa asali kuweka tarehe ya mwisho ya matumizi.

Zipo aina kuu mbili za asali:

  • Asali inayozalishwa na nyuki wadogo (Wasiouma) ambayo inasemekana ni nzuri zaidi kwa sababu nyuki wadogo wanao uwezo wa kuingia kwenye maua madogo ukilinganisha na wakubwa
  • Asali inayozalishwa na nyuki wakubwa (Wanaouma)

Serikali inafanya jitihada gani kuendeleza ufugaji wa nyuki?

  1. Serikali imekuwa ikiandaa maonyesho mbalimbali ya kibiashara na kilimo kama sabasaba na nanenane ambapo wafugaji na wauzaji wameweza kupata fursa za kutangaza bidhaa zao na kupata soko.
  2. Kuanzisha chuo cha ufugaji nyuki (Beekeeping Training Institute) BTI kilichopo manispaa ya Tabora ili kuongeza wataalamu watakaosaidia kutoa mafunzo ya ufugaji nyuki, kuhamasisha na kuelimisha jamii.
  3. Kuwapatia wawekezaji fursa ya kuwekeza katika uzalishaji wa asali ili kuwasaidia wazalishaji wa ndani kupata soko la bidhaa itokanayo na nyuki.

 

Agosti 2017 kampuni ya kijerumani ya QP Tanzania Ltd iliamua kuwekeza katika sekta ya ufugaji nyuki ili kuondoa changamoto ya ukosefu wa soko la asali nchini ikiwa ni kutambua jitihada zinazochukuliwa na serikali katika kuboresha na kuwahakikishia wananchi upatikanaji wa soko hilo.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter