Home VIWANDA “Viwanda 100 kila mkoa” yazalisha viwanda 1,596

“Viwanda 100 kila mkoa” yazalisha viwanda 1,596

0 comment 97 views

Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema hadi kufikia Juni mwaka huu, idadi ya viwanda vilivyojengwa ni 1,596 ambayo ni sawa na asilimia 61.4 ya lengo la kujenga viwanda 2,600 ifikapo mwezi Desemba ikiwa ni utekelezaji wa agizo la ujenzi wa viwanda 100 katika kila mkoa. Majaliwa ametoa takwimu hizo jijini Dodoma wakati akifungua mkutano mkuu wa 34 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT), kwa niaba ya Rais Magufuli.

Waziri Mkuu ameeleza kuwa viwanda hivyo vimejengwa kupitia agizo la Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) la kila mkoa kujenga viwanda 100. Majaliwa ameongeza kuwa tathmini ya utekelezaji wa mkakati wa serikali kuelekea uchumi wa viwanda, inaonyesha kuwa hadi sasa, jumla ya hekta 367,077 zimetengwa katika Mamlaka za serikali za mitaa maalum kwa viwanda vikubwa, vya kati na viwanda vidogo.

“Nitoe wito kwenu kwamba muendelee kupiga hatua nyingine mbele zaidi katika hili, tujue katika hekta hizo zilizotajwa ni kiasi gani kimerasimishwa kwa viwanda vipi, bidhaa zipi zinazalishwa, hali ya miundombinu ikoje na kuna mikakati gani ya kuiendeleza. Pia tufahamu ni ajira ngapi zilizozalishwa kutokana na uanzishwaji wa viwanda hivyo”. Amesema Majaliwa.

Mbali na hayo, Waziri Majaliwa pia ametoa wito kwa viongozi na wasimamizi kuimarisha na kuendeleza sekta ya viwanda ili taifa liweze kutimiza malengo na kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

“Tumieni asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri kuwawezesha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kupitia vikundi vyao ili wawekeze katika viwanda vidogo vidogo vyenye kuleta tija na kuongeza pato la kaya ili kutokomeza umaskini”. Amesisitiza Majaliwa.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter