Home BENKI Benki tano zafungiwa ubadilishaji fedha

Benki tano zafungiwa ubadilishaji fedha

0 comment 94 views

Siku chache baada ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuendesha ukaguzi wa ghafla katika maduka ya kubadili fedha za kigeni jijini Arusha, BoT imezipiga marufuku benki tano za biashara kuendesha biashara ya ubadilishaji fedha za kigeni kwa muda wa mwezi mmoja kuanzia Novemba 23 kwa madai ya kukiuka Sheria. Katika maelezo yake, Mkurugenzi wa masoko ya fedha kutoka Benki kuu, Alexander Mwinamila ametaja benki zilizokumbwa na marufuku hiyo kufuatia kukiuka Sheria za Biashara kuwa ni pamoja na Benki ya Barclays Tanzania, Exim Bank, UBA Bank, BancABC na Azania Bank.

“Hatua hii imetokana na kuvunjwa kwa taratubu na kanuni, waliofungiwa walikuwa aidha wanafanya biashara kinyume na viwango vinavyowekwa au walikuwa hawawasilishi taarifa za miamala waliyokuwa wanafanya”. Ameeleza Mkurugenzi huyo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa biashara kutoka benki ya Azania Gilbert Mwandimila amesema changamoto za teknolojia zilipelekea kuchelewa kwa ripoti kuhusu biashara ya fedha na kueleza kuwa, marufuku waliyopewa itaathiri kwa kiasi kikubwa uwezo wa benki kutoa huduma kwa wateja. Aidha, benki ya Barclays Tanzania imedhibitisha taarifa za marufuku hiyo na kusema itashirikiana na BoT kutafuta ufumbuzi wa suala hilo.

Wiki mbili zilizopita, BoT ilifungia maduka kadhaa jijini Arusha kwa makosa ya kuendesha shughuli zake bila kufuata utaratibu wa Sheria zinazosimamia biashara hiyo na baadae kutangaza kuwa huduma za ubadilishaji fedha zitapatikana katika hoteli za kitalii, benki pamoja na ofisi zao.

 

 

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter