Mkurugenzi wa Fedha wa Benki ya Biashara ya DCB, Zacharia Kapama amesema benki hiyo imefanya jitihada kubwa kuhakikisha inatoka kwenye hasara waliyoipata mwaka 2017, ambapo mpaka sasa imetangaza kupata faida ghafi ya Sh. 1.9 bilioni. Faida hiyo imetokana na mapato halisi ya riba kuimarika na uboreshaji wa huduma za mfumo wa kidigitali ambazo zimeongeza idadi ya wateja kutoka maeneo mbalimbali nchini kote.
“Benki imefanya juhudi za makusudi kuhakikisha inatoka kwenye hasara iliyopatikana mwaka 2017 na kurudi kwenye faida baada ya kuchukua hatua kadhaa ikiwemo ya kuongeza kasi ya ukusanyaji madeni. Mikopo ya jumla ya Sh. 65 bilioni imetolewa mwaka 2018 na kati ya fedha hizo Sh. 21 bilioni ilitolewa kwa wajasiriamali wadogo. Tumeongeza uboreshaji wa mifumo ya uendeshaji biashara kupitia mfumo wa kijidigitali na mkazo ukiwekwa katika kuongeza amana za gharama nafuu kupitia bidhaa za amana za kijiditali na usimamizi wa mizania wenye ufanisi”. Amefafanua Kapama.
Naye Mkurugenzi wa Biashara wa DCB, James Ngaluko amesema waliongeza kasi ya kiutendaji na kuchangia upunguaji wa gharama za uendeshaji kutoka Sh. 21.2 bilioni mwaka juzi hadi kufikia Sh. 16.9 bilioni mwaka jana.
“Huduma za kidigitali zimekuwa chachu ya kuongeza ufanisi na kupunguza gharama za uendeshaji na gharama za riba, hizi ni kama vile akaunti kidijiti, DCB kibubu digitali na DCB FDR digitali akaunti. Akaunti hizi zinamuwezesha mteja kufungua akaunti na kufanya miamala yote ya kibenki, kutunza pesa na kuwekeza kwa kutumia simu yake ya mkononi”. Ameeleza Mkurugenzi huyo.