Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema mchango wa sekta ya kilimo katika kuleta mageuzi ya kiuchumi hapa nchini ni mkubwa ikiwa changamoto kama za upatikanaji wa pembejeo, miundombinu duni ya uzalishaji, usafirishaji, uchakataji mazao na masoko zitashughulikiwa kwa wakati.
Majaliwa ameeleza hayo wakati akifungua ofisi ya Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) Kanda ya Ziwa. Ametoa wito kwa benki hiyo kushirikiana na wadau mbalimbali ili kutatua changamoto hizo na kufanikisha nchi kufikia uchumi kati ifikapo mwaka 2025.
“Endeleeni kufanya kazi na wadau mbalimbali kwa ajili ya kuweka na kutekeleza mipango ya utatuzi wa changamoto zinazowakabili wakulima, wafugaji na wavuvi nchini. Pia panueni zaidi wigo wa huduma hususani utoaji wa mikopo katika kuendeleza miradi ya miundombinu ya kilimo, ufugaji na uvuvi na kutoa mafunzo kwa wakulima wadogo kwa lengo la kuinua uzalishaji”. Amesema Majaliwa.
Wakati huo huo, Naibu Waziri wa Kilimo, Innocent Bashungwa amesema uwepo wa TABD Kanda ya Ziwa utasogeza huduma karibu zaidi na wakulima. Vilevile, ameagiza benki hiyo kuja na mchakato wa kuwafundisha wakulima jinsi ya kuandika maombi ya mikopo.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya TADB, Japhet Justine amesema hadi kufikia Februari mwaka huu, wamefanikiwa kukuza mtaji wa benki hadi Sh. 68 bilioni kutoka ule wa Sh. 60 bilioni uliotolewa na serikali mwaka 2015.
“Kilimo ‘kinabenkika’ kwani katika msimu wa pamba wa mwaka 2018 TADB ilitoa mkopo wa gharama nafuu ili kufanikisha ununuzi na usambazaji wa viuatilifu vya zao la pamba kwa wakulima katika mikoa 17 ikiwemo yote ya Kongani ya Kanda ya Ziwa na wilaya 49 nchini”. Ameeleza Justine.