Home BIASHARABIASHARA NDOGO NDOGO Biashara 5 za kufanya kama una mtaji mdogo

Biashara 5 za kufanya kama una mtaji mdogo

0 comment 510 views

Watu wengi hufikiria namna wanaweza kubadilisha maisha yao hususani katika upande wa kiuchumi na katika biashara au kazi wanazozifanya au wanafikiria kuzifanya. Vitu mbalimbali vinaweza kukuvunja moyo wa kutimiza malengo yako. Unachotakiwa kufanya ni kuwa jasiri na kuendelea kupambana ili uweze kufika unapotaka. Unaweza kunipa sababu kwamba huwezi kushughulikia fursa mpya kwa sababu hauna kipato. Lakini je unafahamu kuwa, si kila biashara inahitaji mamilioni kuanzisha?

Zipo biashara nyingi zinazohitaji mtaji mdogo tu. Ni kama hizi zifuatazo:

Manunuzi ya mahitaji ya nyumbani

Watu wengi siku hizi hawana muda wa kwenda sokoni na kufanya manunuzi ya mahitaji ya nyumbani. Hivyo unaweza kutumia fursa hiyo kujipatia fedha. Unachohitaji ni usafiri inaweza kuwa usafiri wa pikipiki au bajaji kwa sababu lengo hapa ni wewe upate faida hivyo huhitaji kutumia fedha nyingi kwenye usafiri. Angalia usafiri utakaokufaa ambao ni wa bei nafuu, tafuta soko ambalo lina bidhaa za bei nafuu, tengeneza mahusiano mazuri na wafanyabiashara wa bidhaa ambazo utakuwa unazinunua, unaweza kutengeneza akaunti kwenye mitandao ya kijamii ili watu waweze kujua zaidi kuhusu huduma unayotoa, usisite kuwaambia  ndugu na marafiki ili waweze kuwaambia watu wengine. Watu wakiridhika na huduma, basi utaona muelekeo mzuri katika biashara utakaokuletea faida na maendeleo.

Biashara ya chakula

Kila mmoja anajaribu kupambana na maisha ili kufikia malengo yake. Hivyo basi muda mwingi wanajali mambo mengine na kuipa kipaumbele kidogo afya. Watu wengi hupuuza vyakula vinavyoimarisha afya hadi pale watakapoona mabadiliko katika miili yao. Hii ni fursa kwako, Vyakula rafiki kwa afya bora huuzwa bei ya kawaida masokoni hivyo kwa kuanza unaweza kuanza biashara hii nyumbani hadi pale watu watakapoizoea na wewe ukiwa na uwezo wa kuwa na sehemu maalum. Biashara hii inakupasa kuwa mbunifu na kuzingatia usafi. Jifunze kila siku kupitia mitandao au vitabu. Tafuta namna nafuu ya kupata mahitaji yako.

Usafi

Kama unapenda kufanya usafi basi unaweza kujipatia kipato kizuri tu kupitia kitu unachofurahi kufanya bila gharama kubwa. Cha muhimu ni umakini na watu kujua kwamba unafanya shughuli hiyo. Unachotakiwa kufanya ni kuwa na ratiba, vifaa unaweza kuwa navyo wewe mwenyewe au unaweza kumuelekeza muhusika vitu utakavyohitaji ili kukamilisha usafi, unaweza kuwa na msaidizi kulingana na nyumba unayoenda kusafisha au kutokana na kazi unazopata kwa siku. Kazi ikiendelea kukua unaweza kuongeza wasaidizi na kuwaelimisha kuhusu shughuli hiyo ili wasifanye kazi tofauti na inavyotakiwa. Uaminifu ni muhimu sana kwenye kazi kama hii.

Shule ya watoto (Daycare)

Hii ni fursa kubwa hasa kwa wale ambao hawana kazi, na wanapenda sana watoto. Anza kidogo kidogo mtaani kwenu. Waeleze wazazi ambao wanafanya kazi au biashara kuwa unaweza kuwaangalia watoto wao hadi pale watakaporudi kwa kiasi kidogo cha fedha kwa ajili yako na itategemeana kama wanahitaji kuchangia fedha ya chakula au ni bure. Wasisitizie wakupe fedha ya tahadhari kama jambo lolote litatokea. Fedha hiyo usiitumie kwa mambo yako binafsi. Pia usifanye mambo mabaya ambayo yanaweza kuwaathiri watoto hao kwa namna yoyote ile wakiwa chini ya uangalizi wako. Weka ratiba, buni njia mbalimbali za kuwaelimisha, na kuwafanya wafurahi kuwa kwenye uangalizi wako, kwa sababu watoto wadogo hupenda kudadisi na  kujifunza. Idadi ikiongezeka inafaa utafute sehemu maalum na ufuate Sheria zinazoelekeza biashara hiyo.

Kutafsiri

Kama unajua lugha zaidi ya moja, basi unaweza kujipatia fedha kupitia ufahamu huo. Unaweza kujitambulisha katika taasisi zinazohusika na mambo ya utalii, si lazima wakuajiri, wanaweza kuwa wanakutumia pale wanapokuhitaji hii itakusaidia pia kufanya shughuli zako nyingine. Mahusiano mazuri kwa wale utakaokuwa unawafanyia tafsiri hizo ni muhimu ili warudi tena mara nyingine wakihitaji huduma.

Fursa ni nyingi sana katika maisha yetu. Suala la muhimu ni kuwa na utayari na kuamua kufanyia kazi jambo fulani. Ukipenda kitu ni rahisi kuchukua hatua na kukifanya kwa asilimia mia moja. Utayari ndio dhana yako ya kubadilisha maisha. Watu wengine wasikutishe na maendeleo yao. Ni muhimu kuwa mvumilivu na kuendelea kujifunza kila siku bila kukata tamaa ili kutoa huduma nzuri kwa wateja wako.

 

Leave a Comment

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter