Home FEDHA Njia rahisi za kubana matumizi

Njia rahisi za kubana matumizi

0 comment 129 views

Suala la bajeti limeendelea kuwa gumu kwa watu wengi. Kutokuwa na malengo ni moja ya sababu inayopelekea hali hii. Sio vibaya kama ukitumia fedha zako kupata kila unachotaka lakini ni muhimu kuwa na mpangilio ambao utakuhakikishia utapata mahitaji yako ya kila siku. Heshima katika fedha unayojipatia kila mwezi, kila wiki au kila siku ni muhimu kwa sababu ukikosa heshima hiyo, hutakuwa na muelekeo.

Hapo chini ni njia rahisi ya kugawanya kipato chako/mshahara na kuweka bajeti

Kwanza kabisa, ni muhimu kugawanya mshahara/kipato chako katika makundi matatu: Malengo ya kifedha ya muda mrefu, ya muda mfupi na gharama za kumudu maisha.

MALENGO YA KIFEDHA YA MUDA MREFU

Hapa unashauriwa kuweka bajeti si chini ya asilimia 20 ya mshahara/kipato chako kwani kupitia malengo haya utategemea kuongeza kipato zaidi na kujiletea maendeleo. Malengo ya muda mrefu yanaweza kuwa, kuanzisha biashara, kununua kiwanja aidha kwa ajili ya kuuza baadae thamani yake ikiongezeka au kwa ajili ya kujenga, kuwekeza katika hisa, soko la fedha za kigeni au soko la dhamana (bonds).

MALENGO YA KIFEDHA YA MUDA MFUPI

Mara nyingi watu hupuuzia bajeti ya malengo ya muda mfupi, hivyo kujikuta wanatumia fedha nyingi zaidi katika malengo haya. Ni muhimu kuwa na mfumo katika kila kitu hivyo katika malengo haya unaweza kuweka asilimia ndogo tu na kuhakikisha hutumii zaidi ya hapo. Malengo ya muda mfupi yanaweza kuwa kama kutembelea vivutio, kusafiri, kwenda likizo, kununua nguo, viatu, kukutana na marafiki katika maeneo ya starehe na kadhalika.

GHARAMA ZA KUMUDU MAISHA

Hapa ni muhimu ukiweka bajeti kubwa ili kuondokana na changamoto zinazoweza kutokea katika maisha ya kila siku kwa mfano kudaiwa kodi, kuweka mafuta kwenye gari, nauli, chakula na bima. Katika hili, tumetofautiana kuna watu wana gharama kubwa za kushi na wengine wana gharama ndogo za kuishi hivyo kama una gharama ndogo za kuishi unashauriwa kuweka fedha zaidi katika malengo yako ya muda mrefu.

Mfano wa mishahara miwili tofauti na mgawanyo wa fedha:

  1. Irene

Mshahara kwa mwezi: 1,000,000 Tsh

Malengo muda mrefu (20%): 200,000/=

Malengo muda mfupi (10%): 100,000/=

Gharama za kuishi (70%): 700,000/=

*Irene amepanga, ana gari ambalo linahitaji mafuta na vilevile anajitegemea chakula kazini kwake.

2. Lilian

Mshahara kwa Mwezi: 800,000 Tsh

Malengo ya muda mrefu (20%): 160,000/=

Malengo ya muda mfupi (10%): 80,000/=

Gharama za kuishi (70%): 560,000/=

*Lilian anakaa kwao, anatumia gari ya ofisini na fedha ya mafuta inatolewa na ofisi, pia ofisi inamlipia chakula.

Hapa Lilian anashauriwa kuwekeza zaidi kwenye malengo ya muda mrefu kwa sababu ana gharama ndogo ya kuishi.

 

 

 

Leave a Comment

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter