Na Mwandishi wetu
Akiwa katika mazungumzo na waandishi wa habari, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Simba Cement, Reinhardt Swart amesema viwanda vya saruji nchini vinakumbana na changamoto kubwa za usafirishaji baada ya serikali kuagiza viwanda hivyo kutumia makaa ya mawe yanayochimbwa ndani ya nchi. Swart amesema ubora wa makaaa hayo ya mawe unaridhisha lakini gharama za usafirishaji zipo juu sana.
Akitolea ufafanuzi zaidi kuhusu suala hili, mkurugenzi huyo amesema kampuni yake ya Simba Cement inatumia tani 12,000 za makaa ya mawe kwa mwezi mmoja, hivyo malori zaidi ya 400 yanahitajika kubebea tani 30 kutoka Ngaka Ruvuma hadi Tanga kila siku.
Saruji ya kutosha imekuwa ikizalishwa hapa nchini na hali hiyo imepelekea viwanda hivyo kupeleka bidhaa zao nchi za nje ambapo kuna ushindani mkubwa kutoka kwa nchi zilizoendelea.
Simba Cement imekuwa ya kwanza kusajiliwa katika Soko la Hisa la Dar es salaam (DSE) kwenye sekta ya saruji na kwa kipindi cha miaka sita kampuni hiyo imelipa kodi ya mapato zaidi ya Sh 252 bilioni hivyo Swart ameomba serikali kuangalia namna ya kupunguza gharama hizo katika sekta ya saruji ili iendelee kufanya vema.