Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji ametoa pongezi kwa benki ambazo zimeitikia wito wa serikali na kupunguza viwango vyao vya riba ili kuimarisha uwezo wao wa kukopesha wateja. Dk. Kijaji amesema hayo wakati akifunga warsha ya wadau wa sekta ya fedha iliyowashirikisha wabunge, washirika wa maendeleo, wakuu wa taasisi za fedha pamoja na Wizara ya Fedha na Mipango.
Miongoni mwa benki zilizoshusha viwango vya riba za mikopo ni CRDB ambayo imetangaza kushusha riba kutoka asilimia 22 hadi 16 na kuongeza kiasi cha kukopa kwa wafanyakazi kutoka Sh. milioni 50 hadi Sh. milioni 100 huku muda wa kurejesha mikopo hiyo ukiongezwa kutoka miaka mitano hadi saba. Benki nyingine ni NMB ambayo imeongeza muda wa marejesho ya mikopo kwa wafanyakazi na wajasiriamali kutoka miezi 60 hadi 72, na kupunguza riba ya mikopo kwa wafanyakazi kutoka asilimia 21 hadi 19 na wajasiriamali wadogo kutoka asilimia 23 hadi 21.
Naibu Waziri huyo amezipongeza benki zilizoshusha viwango vya riba na kusema hatua hiyo ni muhimu katika kuifikisha Tanzania kuwa nchi ya viwanda hata kabla ya mwaka 2025. Vilevile ametoa wito kwa taasisi za fedha kuangalia sekta ya kilimo kwani ina mchango mkubwa katika kutimiza malengo ya kukuza viwanda.