Home BENKI BoT, Citibank wajadili mikopo chechefu

BoT, Citibank wajadili mikopo chechefu

0 comment 178 views

Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Emmanuel Tutuba, amekutana na Mkuu wa Kundi la Citibank Kusini mwa Jangwa la Sahara, Akin Dawodu jijini Dodoma kuzungumza masuala mbalimbali yanayohusu sekta ya fedha.

Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Mei 28, 2024, Gavana Tutuba amesema utendaji wa Citibank umeonesha kuongezeka kwa faida na kupungua kwa kiasi kikubwa kwa mikopo chechefu.

Amemweleza Dawodu kwamba Mtendaji Mkuu wa Citibank Tanzania, ambaye pia alishiriki kikao hicho, Geofrey Mchangila, amekuwa akifanya kazi vizuri sana katika sekta ya fedha nchini hata kuaminiwa kuwa kiongozi kwenye Jumuiya ya Mabenki Tanzania.

“Tunafurahia utendaji wenu wa kazi, hatuhitaji kutumia nguvu nyingi kuwasimamia. Mnafanya vizuri sana, na kwenye mikopo chechefu tunashauri benki nyingine zije zijifunze kwenu jinsi mlivyofanya,” alisema.

Pia, Gavana aliishauri Citibank ambayo mwaka kesho inatarajia kuadhimisha miaka 30 tangu ianze biashara hapa nchini, kufikiria kusogeza huduma zao katika maeneo mengine na kuanza kuhudumia wateja binafsi badala ya kujikita kwa wateja wa kitaasisi.

Kwa upande wake, Dawodu ameeleza utayari wa benki yake kuendelea kufanya kazi na mamlaka za Tanzania katika kuendeleza sekta ya fedha.

“Mwaka kesho tunaadhimisha miaka 30 tangu tuingie hapa Tanzania. Tunatarajia kuendelea kuwepo kwa miaka mingine 30. Tunahitaji msaada tunapozidi kusonga hatua nyingine,” amesema.

Viongozi hao wawili pia walijadili masuala mbalimbali ya faida kwa pande zote mbili pamoja na yanayohusu kukuza sekta ya fedha kwa ujumla hapa nchini.

Mkurugenzi wa Usimamizi wa Sekta ya Fedha, Sadati Musa, Kaimu Meneja wa Usimamizi wa Mabenki, Neema Koka, Kaimu Mkurugenzi wa Utafiti na Sera za Uchumi, Dkt. Deogratias Macha na Msaidizi wa Gavana, Dkt. Mosses Mwizarubi, walishiriki katika kikao hicho kwa upande wa Benki Kuu.

Kundi la Citibank linatoa huduma zake katika nchi 95 duniani.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter