Baada ya kumaliza kipindi chake cha miaka minne kuongoza benki ya NMB, Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Ineke Bussemaker ametoa pongezi kwa serikali kwa namna iliyoshirikiana naye kipindi chote cha uongozi wake. Bussemaker amesema hayo katika hafla ya kumuaga rasmi iliyofanyika jijini Dar es salaam ambapo mbali ya kuishukuru serikali, Mkurugenzi huyo pia amewashukuru watanzania na kusema wamemuwezesha kufanya kazi kwa mafanikio.
Katika hafla hiyo, watendaji mbalimbali kutoka taasisi nyingine pia walishiriki kumuaga Bussemaker ambapo Mkurugenzi huyo alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa wafanyakazi wa benki ya NMB kufanya kazi kama timu moja. Bussemaker ameeleza kuwa, benki hiyo imepata mafanikio ikiwemo kufungua matawi mapya ambapo hadi sasa NMB ina jumla ya matawi 228 nchini kote, mashine za kutoa fedha (ATM) takribani 800 pamoja na mawakala wapatao 6,000. Aidha, chini ya uongozi wake, benki ya NMB imefanikiwa kuzindua matumizi ya kadi za Mastercard ikiwa ni mojawapo ya mikakati ya benki hiyo inayolenga teknolojia na ubunifu.
“Naomba jamii kufanya biashara na sisi kwa ajili ya maendeleo ya viwanda na kuwawezesha wanawake katika awamu hii ya tano”. Amesema Bussemaker.