Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji amesema serikali inafanya mazungumzo na serikali ya Cyprus ili kutatua changamoto ya wateja wa FBME ambao waliweka dhamana kwenye benki hiyo iliyofutiwa leseni na Benki Kuu ya Tanzania (BoT). Dk. Kijaji amesema hayo bungeni Dodoma wakati akijibu swali la Asha Abdallah Juma, (Mbunge Viti Maalum) aliyehoji hatua zilizochukuliwa na serikali kuwasaidia wananchi waliokumbwa na tatizo hilo.
Katika maelezo yake, Naibu Waziri huyo amesema mchakato wa ukusanyaji mali pamoja na fedha za benki hiyo katika taasisi mbalimbali hususani za nje ya nchi limekuwa na changamoto za kisheria baina ya Tanzania na Cyprus ambapo FBME imekuwa ikiendesha sehemu kubwa ya biashara zake, hali ambayo imepelekea zoezi la makusanyo na ugawaji wa fedha za ufilisi kuchukua muda mrefu.
“Hakuna tarehe rasmi ya kuanza kulipa fedha kwa sasa kutokana na uwepo wa kesi zinazokwamisha zoezi la ukusanyaji mali na madeni ya benki ya FBME”. Amefafanua Dk. Kijaji.
Pamoja na hayo, Naibu huyo amewaeleza wabunge kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Benki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2016, amana au akiba za wateja zina kinga ya bima ya amana iwapo kiasi cha fedha ni chini ya Sh. 1.5 milioni na ikitokea mteja na kiasi salio la amana chini ya Sh. 1.5 milioni, faida yake ni asilimia 100. Kwa upande wa wateja wenye kiasi kinachozidi Sh. 1.5 milioni, watalipwa Sh. 1.5 milioni kama fidia wakati kiasi kinachosalia kikilipwa wa mujibu wa Sheria za ufilisi.