Home BENKI NMB Benki kutengeneza ajira 50 kupitia mafunzo kazini

NMB Benki kutengeneza ajira 50 kupitia mafunzo kazini

0 comment 77 views

Benki ya NMB kutengeneza fursa za ajira kwa wahitimu wa vyuo vikuu zaidi ya 50 kupitia programu yake maalum ya mafunzo ya vitendo kazini iliyoanzishwa takribani miaka 10 iliyopita.

Mbali na kutoa fursa kwa wahitimu wasio na kazi na sifa zinazohitajika kuajiriwa moja kwa moja, uwekezaji huo umeiwezesha NMB kuzalisha wafanyakazi wenye ujuzi na weledi mkubwa katika maswala ya kifedha na kibenki.

Akizungumza wakati wa mahafali ya wahitimu watano wa mwaka huu wa programu hiyo, Ofisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa NMB, Filbert Mponzi, alisema mchakato huo si muhimu tu kwa benki hiyo na washiriki wake bali pia kwa tasnia ya fedha na nchi kwa ujumla.

Mahafali hayo yalifanyika makao makuu ya NMB jijini Dar es Salaam na tayari zoezi la kupata wanafunzi wengine 10 watakaoanza mafunzo hayo mapema mwakani yanayochukua miaka miwili limekamilika.

“Kama benki inayoongoza kwa faida nchini, tunalo lengo lakutatua changamoto mbalimbali zinazowakumba vijana hususani kwenye masuala ya ajira nchini, hivyo vijana hawa tuliwachukua walivyomaliza kozi mbalimbali vyuoni na kuwapa ujuzi katika maeneo ya kazi ili waweze kuwa na uzoefu wanapoajiriwa,” alifafanua Mponzi.

Mgeni rasmi katika mahafali hayo Margaret Ikongo ambae ni Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa NMB, aliyewapongeza wahitimu kwa kuzishinda changamoto walizokumbana nazo baada ya masomo vyuoni.

Alisema hiyo ni mojawapo ya sababu zilizochangia utendaji wao bora na ufanisi kazini mpaka kuajiriwa moja kwa moja na NMB.

“Jinsi mlivyofanya kazi kwa bidii, uvumilivu, juhudi, maarifa, nidhamu na kujituma kipindi cha mafunzo ya  miaka miwili, naomba msiishie hapa tu, bali muende mkalete mapinduzi kwenye kila kazi mnayogusa ili benki yetu iendelee kusonga mbele,” aliwambia wahitimu hao.

Kwa niaba ya wahitimu wenzake, Agnes Nyanzala, alikiri kuyafurahia mafunzo ya vitendo kwa miaka miwili, yaliyojaa uwezeshaji uliowapa urahisi wa kiutendaji, kiasi cha kuivutia NMB na kuwapa ajira.

Nyanzala alisema kuwa kwa sasa wameiva vya kutosha na wana ari kubwa katika kufanya kazi kwa bidii, maarifa na weledi na kwamba wako tayari kwa mamapambano ya kunyanyua ustawi wa NMB kuanzia mwaka ujao wa 2021.

Programu ya mafunzo kazini ya NMB ilianzishwa mwaka 2009 na kila baada ya miaka miwili benki hiyo huwatuma wataalamu wake wa rasilimali watu kwenda vyuoni kutafuta wanafunzi wenye vipaji wapate mafunzo ya vitendo ndani ya benki.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter