Home BENKI TADB kuwafuata wakulima vijijini

TADB kuwafuata wakulima vijijini

0 comment 99 views

Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania(TADB) imeanza kupanua huduma zake kwa kufungua matawi katika kanda mbili jijini Mwanza na Dodoma. Uamuzi huo umekuja kufuatia agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Magufuli la kuitaka benki hiyo kufungua matawi yake vijijini ili kuwasaidia wananchi hasa wakulima wadogo kupata huduma ya benki vijijini ikiwa ni pamoja na mikopo.

Rais Magufuli alitoa agizo hilo alipozindua Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo awamu ya pili (SADP II) ambapo alitoa wito kwa TADB kujikita kukopesha wakulima badala ya kukopesha benki.

Akizungumza katika Maonyesho ya 42 ya biashara ya kimataifa (Sabasaba), Mkurugenzi wa Fedha na Tehama wa TADB Severin Ndaskoi alisema kuwa wameshaanza kutekeleza agizo hilo kwa kufungua matwi yao katika kanda ya mikoa hiyo ili kuwafikia wananchi kwa urahisi.

“Katika mikoa hiyo ofisi na kila kinachohitajika ikiwemo wafanyakazi vipo tayari,bado kufungua rasmi lakini shughuli ndogondogo zimeshaanza” Alisema Ndaskoi.

Ndaskoi alidai kuwa kutokana na uchanga wao hawawezi kumudu kufungua matawi nchi nzima lakini watashirikiana na benki nyingine kuwasaidia wananchi kwa kutoa dhamana.

“ Wakulima hawakopesheki kwa urahisi kutokana na baadhi ya benki kuogopa hatari iliyopo kwenye kilimo, hivyo kwa kuwasaidia tunawapa dhamana wao wanatoa asilimia 50 na sisi 50 ili wakopesheke” Alifafanua Ndaskoi.

Aidha Mkurugenzi huyo amedai hadi mwisho wa mwaka huu, TADB itakuwa imefungua matawi yake katika mikoa minne ikiwemo Kigoma, ikiwa ni pamoja na utoaji wa mikopo yenye jumla ya Tsh. 45 bilioni kutoka bilioni 11 zilizokopeshwa mwaka jana.

Kwa upande wake, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango amesema anataka benki hiyo kuongeza kasi na kuwafikia wakulima.

“ Sitaki kuiona hii benki mijini, nataka ijitanue zaidi walipo wakulima.” Ameagiza Dk. Mpango

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter