Home BIASHARA Kongamano la kwanza la kikodi nchini lakutanisha wadau

Kongamano la kwanza la kikodi nchini lakutanisha wadau

0 comment 19 views

Serikali kupitia Wizara ya Fedha imefanya kongamano la kodi kikanda kwa kuwakutanisha Wadau kutoka sekta binafsi wakijumuisha wataalam na washauri wa kodi, wadau wa sekta mbalimbali nchini, wafanyabiashara, wazalishaji wa bidhaa na mazao mbalimbali pamoja na Makundi Maalum ili kuboresha mifumo ya kodi itakayochochea mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji nchini.

Hayo yameelezwa na Kamishna Msaidizi Idara ya Sera William Mhoja, katika kongamano la kwanza la kodi kikanda kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026, lililofanyika jijini Dodoma.

Mhoja alisema kongamano hilo litasaidia kuboresha uratibu wa ukusanyaji maoni na kuongeza ushirikishwaji wa makundi mbalimbali katika uandaaji wa bajeti ya Serikali na utunzi wa sheria.

“Hatua hii ni moja ya utamaduni wa kutambua mchango wa wananchi kupitia kodi, ada na tozo mbalimbali ambazo zinawezesha ujenzi wa Taifa letu,” amesema,Mhoja.

Amesema kuwa lengo la kongamano hilo lilikuwa kupata maoni mbalimbali kwa nchi nzima ikiwa ni pamoja na kupita kwenye Kanda ikiwemo Kanda ya Dodoma ambayo ukusanyaji maoni umenza, Arusha, Mwanza, Kigoma, Mbeya, Iringa na baadae Mtwara na kuhitimisha zoezi hilo Dar es Salaam.

Amesema kuwa katika kongamano hilo maoni yote yatakayotolewa na wadau mbalimbali yatafanyiwa kazi ikiwa ni pamoja na kuyafanyia utafiti kabla ya kufanyiwa utekelezaji.

“Hivyo Serikali inawaahidi kwamba maoni yao yanazingatiwa sana kama ambavyo mmeona katika Hotuba za bajeti na Serikali inawakaribisha sana kushiriki na kutoa maoni. Kimsingi maoni ya wananchi wote yanazingatiwa na nawaomba sana wananchi wote wajitokeze kutoa maoni na maoni yao yatafanyiwa kazi kwa sababu mengine yanahitaji kufanyiwa utafiti kwanza kabla ya kuyaleta kwenye utekelezaji,” ameeleza Mhoja.

Aidha, amewashukuru Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA) pamoja na TradeMark Afrika kwa kushirikiana na Serikali hususan katika kudhamini baadhi ya shughuli mbalimbali katika makongamano haya.

“Ni wazi kuwa ushirikiano huu unalenga kuendelea kukuza uchumi, kuzalisha ajira zaidi na kuwa na maendeleo endelevu,” amesisitiza Mhoja.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter