Kampuni ya kimataifa ya kuhudumia shehena ya kontena bandarini (TICTS), ikiwa kama kampuni pekee ya huduma kwa kontena inayofanya kazi katika bandari kubwa nchini Tanzania imefikia hatua mpya ya mafanikio na kuweka rekodi mpya ya kuhudumia shehena ya kontena 592,000 katika mwaka 2018. Rekodi ya mwisho iliwekwa na kampuni hiyo mwaka 2017 ambapo ilihudumia kontena 502,690. Katika mwaka wa 2018, TICTS pia iliweka rekodi ya mwezi katika mwezi wa Agosti kwa kuweza kuhudumia kontena 54,447 na rekodi ya kontena 31, 239 zilihudumiwa katika mageti katika mwezi Machi 2018.
Ongezeko la shehena ya ndani na kwa ajili ya nje ya nchi imeongezeka kwa asilimia 18, zaidi ya mwaka 2017. Mizigo ambayo ni kwa nchi mbalimbali zinazotumia bandari yetu iliongezeka kwa wastani zaidi ya asilimia 38.9 kwa mwaka 2018. Ongezeko la shehena linahitaji ufanisi na uharaka katika utoaji mizigo ili kupunguza muda wa mizigo kukaa bandarini na hivyo kuwezesha TICTS na Bandari kuongeza ufanisi na uwezo wa kuhudumia shehena kubwa zaidi. Kampuni imefanikiwa ukuaji huu licha ya changamoto za mazingira ya kibiashara kimataifa na katika kanda.
Afisa Mtendaji Mkuu, Jared Zerbe alisema, ‘’Msaada na ushirikiano tunaopata kutoka kwa Serikali ya Tanzania, Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Mamlaka ya Mapato (TRA),wafanyakazi wetu, wateja na wadau wanaotumia bandari hii ndio imekua chanzo cha ukuaji wa huduma za TICTS katika mwaka 2018. Binafsi najivunia sana kwa timu yetu nzuri sana wakipambana na changamoto ya kuhudumia ongezeko la shehena.’’
Kuongeza ufanisi ili kuweza kuhudumia shehena hii inayokua, TICTS itaendelea kufanya kazi na Serikali ya Tanzania, TPA, TRA na wateja na kufanyia kazi changamoto zote zinazoathiri utolewaji haraka wa mizigo katika bandari Dar es Salaam.