Home BIASHARA Ukiendekeza haya hutofanikiwa

Ukiendekeza haya hutofanikiwa

0 comment 104 views

Watu wengi huamini kuwa mafanikio ni matokeo ya kufanya kazi kwa bidii tu bila la kuzingatia vipengele vingine muhimu. Ukweli ni kwamba waliofanikiwa hawakuwekeza kwenye kufanya kazi kwa bidii peke yake bali waliweka jitihada kuacha tabia ambazo zilikuwa zinawakwamisha kutimiza malengo yao.

Ikiwa wewe unataka kufanikiwa, epuka tabia zifautazo:

Ahadi za uongo

Ikiwa wewe mwenyewe unashindwa unashindwa kutimiza ahadi basi unaweka jina lako pamoja na lile la kampuni au biashara yako katika nafasi mbaya kwa kuwa hakuna mtu anayependa kufanya kazi na mtu ambaye hatimizi ahadi zake.

Kulaumu watu wengine

Badala ya kujiuliza kwa nini mtu fulani amenifanyia hivi?, Jiulize je tunachukua hatua gani kutatua jambo hili? Kuwa na tabia ya kulaumu watu wengine na kulalamika kuwa wao ni kikwazo cha mafanikio yako sio vizuri. Mafanikio ya kweli hutegemea tabia na mwenendo wako binafsi.

Kusubiri ‘muda muafaka’

Hakuna kitu kama muda muafaka. Tabia ya kusema kuwa unasubiria muda muafaka kuanzisha biashara au mradi fulani ni kisingizo cha kuendelea kutofanya kazi ili kufikia malengo yako. Dhana ya muda muafaka hutokana na uoga wa mtu kuchukua hatua na sio kubaki na mawazo ambayo hayana utekelezaji wowote.

Kuzungumzia malengo bila kuyapangilia

Kama unajikuta unazungumza na rafiki au ndugu yako kuhusu malengo uliyonayo na baada ya miezi kadhaa unajikuta hujafanya chochote kuonyesha maendeleo ya mipango hiyo, muda wa kubadili tabia yako umewadia.

Kutojiamini

Unapokuwa unataka kuanzisha biashara au kampuni yako mwenyewe unatakiwa kuamini kuwa unaweza kutimiza ndoto zako na utafanikiwa. Unatakiwa kuwa shabiki namba moja wa ndoto zako. Jiamini na chukua hatua ndogo kila siku kufika unapotaka.

Kujilinganisha na watu wengine

Kitu ambacho watu wengi hawafahamu ni kwamba watu wenye mafanikio makubwa leo hii walianza kama wao. Mitandao ya kijamii na magazeti hayazungumzi kuhusu changamoto walizokutana nazo hadi kufanikiwa hivyo jamii inachoamini ni kwamba safari yao ya mafanikio ilikuwa rahisi. Usilinganishe safari yako na ya mtu mwingine kwa kuwa kila mtu anapitia majaribu yake na mazingira hutofautiana

Kupuuza afya yako

Mafanikio na afya bora huenda sambamba. Kama unashindwa kuzingatia afya yako kwa kula chakula bora, kufanya mazoezi na kupumzika basi hata kupata mafanikio itakuwa changamoto kwani huwezi kufanya kazi kwa bidii pasipo kuwa na afya bora.

Kukata tamaa badala ya kujaribu tena

Kwa mtu anayetaka mafanikio hili ni kosa kubwa. Katika maisha kuna changamoto za kila aina lakini kukata tamaa sio suluhisho. Pale unapoona mambo yanakuwa magumu, unaweza kuomba msaada kutoka kwa watu wengine, unaweza kutumia muda wako kufanya utafiti ili kupata njia sahihi ya kutatua matatizo uliyonayo au unaweza kuchukua muda kidogo kupumzika na kujipanga upya. Unapofeli jaribu tena na tena bila kuchoka.

Kusahau umuhimu wa kuendelea kujifunza

Tafuta mbinu za kuendelea kujifunza ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kuenddana na wakati kwa kuwa teknolojia na maisha kwa ujumla yanabadilika. Hata baada ya kuanzisha biashara yako endelea kuwa na moyo wa kujifunza kutoka kwa wengine.

Hivyo basi, ni tabia gani unaweza kubadilisha leo ili kuifanya kesho yako kuwa bora zaidi?

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter