Home BIASHARA Umuhimu wa Logo katika biashara

Umuhimu wa Logo katika biashara

0 comment 322 views

Katika biashara, kuna vitu muhimu ambavyo mjasirimali/mfanyabiashara lazima avizingatie kabla hajaanzisha biashara yake mbali na kuwa na mtaji, vitendea kazi eneo la biashara, soko n.k. Kwa jamii nyingi za Afrika Mashariki, walio wengi wamekuwa wakifanya biashara na biashara zao kufanikiwa kwa kiasi kikubwa tu lakini bado wamekosa kitu kimoja cha muhimu sana.

Wajasiriamali wadogo wadogo na baadhi ya wafanyabiashara hawana nembo zao za biashara maarufu kama Logo.

Nembo ya Biashara (Logo) ni nini na inamsaidia vipi mfanyabiashara/mjasiriamali?

Kwa tafsiri rahisi, nembo ni alama zinazoundwa na maandishi na picha ambazo zinatusaidia kutambua bidhaa au huduma tunayopenda kwa kuwasaidia wateja kuelewa nini unachofanya, wewe ni nani na unaamini nini na matarajio yako ni yapi.

Kuna umuhimu mkubwa wa mfanyabiashara au mjasiriamali kumiliki au kuwa na nembo ya biashara.

Unaweza kuwa na biashara nzuri tu ya utoaji huduma au bidhaa lakini watu wasivutike na biashara yako wakaenda sehemu nyingine kununua kwa sababu tu wamependezwa na nembo ya mfanyabiashara mwenzako kutokana na dhima au ujumbe uliopo.

Kwanini unashauriwa kumiliki au kuwa na nembo ya biashara?

Nembo ya biashara ni utambulisho wako. Kitu kitakachoitambulisha biashara yako au huduma yako bila kujali kama ni bidhaa iko katika uzito au ujazo gani na kama ni huduma haitajalisha inatolewa sehemu gani ni nembo. Nembo inatengeneza hisia, fikra, mwamko na hamasa ya kununua huduma au bidhaa kwa mteja. Kwa mfano ni kawaida kusikia mtu akisema nimeona matangazo ya kampuni fulani kwani imefika hadi huku? Mara nyingi kitu cha kwanza kujiuliza itakuwa ni nembo ya kampuni au biashara.

Nembo inasaidia kuonyesha umaridadi na ufanisi wa kampuni. Kampuni yoyote yenye kuhitaji kufanya kazi kwa ufanisi lazima iwe na logo (nembo). Nembo inasaidia kuonyesha uthubutu na umakini wa kampuni au biashara ambayo yaweza kuwa ni ya utoaji huduma au uzalishaji wa bidhaa.

Nembo inabeba ujumbe wa biashara yako. Ujumbe ni muhimu katika nembo yako kwa sababu inabeba kile ambacho kampuni yako inafanya. Ujumbe mara nyingi huwa ni wenye mvuto na utakaowafanya wateja wako kuvutika na kuja kuhudumiwa au kununua bidhaa zako- Mathalani unamiliki duka la mapambo linaitwa “Mwanamapambo” Kisha ukaweka ujumbe huu “ Unajenga tunakusaidia kupamba” Ujumbe tu umeshabeba kile unachokifanya ambacho ni uuzaji wa mapambo mtu hatokuwa na haja ya kuja kuuliza duka lako linahusiana na mapambo ya aina gani.

Nembo inasaidia kuonyesha umiliki. Nembo ni moja kati ya alama zinazoonyesha umiliki wa biashara kwa sababu nembo hubeba jina la kampuni au mmiliki wa kampuni. Mfano Azam, Kiluswa Company Limited, Kafulusu Enterprises na mengineyo. Majina hayo yanaonyesha mmiliki wa kampuni ni nani.

Nembo inasaidia kuonyesha matarajio ya biashara. Nembo inasaidia kubeba maono na muelekeo wa biashara yako na hasa kwa kuwaonyesha wateja watarajie nini huko mbele kutokana na huduma au bidhaa unazotoa. Hii inasaidia biashara yako kuwa na ushindani dhidi ya kampuni nyingine zinazotoa huduma kama yako. Mfano kampuni za mawasiliano. Maneno kama “Yajayo yanafurahisha! Uko tayari” yanasaidia kuwafanya wateja wa kampuni kuendelea kusubiria mambo mazuri ambayo kampuni yao imewaahidi.

Nembo ya biashara (logo) ina umuhimu mkubwa katika kutambulisha biashara sokoni hivyo ni vema mfanyabiashara au mjasiriamali kuwa na logo kwa sababu itakusaidia kujitofautisha na wafanyabiashara wengine wanaofanya biashara kama yako. Nembo inasaidi sana kuonyesha uthamani wa biashara unayoifanya.

 

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter