Serikali imezitaka Taasisi za Fedha zilizosajiliwa kutoa huduma ya mikopo, kuto wakandamiza wananchi katika mikataba kwa sababu ya kutojua kusoma na kuandika kwa kuwasainisha mikataba bila uelewa wao.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa Wilaya ya Kwimba, Mkoa wa Mwanza Ng’wilabuzu Ndatwa Ludigija, alipokutana na Timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Fedha na Taasisi zake, ambayo ipo mkoani humo kutoa elimu ya fedha kwa wananchi wa makundi mbalimbali.

Baadhi ya wananchi wakishiriki maafunzo ya elimu ya fedha.
“Serikali imesisitiza umuhimu wa uwazi na haki katika mikataba ya kifedha ili kulinda haki za wananchi na kuhakikisha wanajua kikamilifu masharti wanayokubaliana nayo”, alisema Ludigija.
Alifafanunua kuwa Serikali inatambua kuna baadhi ya wananchi hawajui kusoma na kuandika, wamekuwa wakiwekewa miezi mingi zaidi ya marejesho tofauti na walivyokubaliana kwa mdomo.
Ludigija, amewashukuru wataalamu kutoka Wizara ya Fedha kwa kufika mkoani Mwanza kutoa elimu ya fedha kwa kuwa itawasaidia wananchi kuwa na uelewa mpana wa masuala ya fedha ikiwemo kupanga bajeti na kufanya uwekezaji ambao utakuwa na faida kwa kujikwamua kiuchumi.
Afisa Mkuu Mwandamizi, Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha kutoka Wizara ya Fedha Salim Kimaro, aliwasisitiza wananchi kujenga mazoea yakusoma mikataba na kuuelewa kabla ya kusaini.
Aliongeza kuwa baadhi ya wanufaika wa mikopo wanakumbwa na changamoto za marejesho kwa sababu ya kukosa mipango thabiti ya matumizi ya fedha wanazokopa, na wengine hawasomi wala kuelewa mikataba wanayoingia.
Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo Nkwadi Joseph mkazi wa Kwimba aliishukuru Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwaletea wataalamu wa fedha.
“Kabla ya kupata elimu hii, tulikuwa tunaingia kwenye mikopo yenye masharti magumu bila kujua athari zake, sasa tunaelewa umuhimu wa mikopo yenye utaratibu mzuri,” alisema Joseph.
Serikali kupitia Wizara ya Fedha imefanya hitimisho ya kutoa elimu ya fedha kwa wananchi wa makundi mbalimbali katika Wilaya za Ilemela, Magu, Misungwi na Kwimba Mkoa wa Mwanza ambapo hadi sasa Wizara ya Fedha imeshatoa elimu ya fedha katika mikoa 16.