Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti George Simbachawene ametoa wito kwa taasisi za fedha kote nchini kupunguza riba kwenye mikopo wanayotoa kwa vikundi vidogo vidogo ili viweze kujikwamua kiuchumi. Simbachawene amesema hayo alipokuwa akifungua mkutano wa 20 wa Chama cha kuweka na kukopa cha Walimu Mpwapwa.
Mwenyekiti huyo ameeleza kuwa hivi sasa, kinachoonekana kwenye taasisi hizo ni utoaji mikopo yenye riba kubwa jambo linalosababisha ziweze kufa. Simbachawene amesisitiza kuwa lengo kuu la vyama vya ushirika au vile vya kuweka na kukopa fedha ni kuwasaidia wanyonge ambao wanakuwa wameungana kwa dhumuni la kupambana na umaskini.
“Mkopo wenye riba kubwa hauna urafiki na maskini bali una lengo la kudidimiza wanyonge, hizi taasisi zinazotoa mikopo zinatoa kwa riba kubwa jambo linalosababisha zingine kufa, kufilisiwa mali zao”. Amesema Simbachawene.
Kwa upande wake, Meneja wa chama hicho, Joackim Mokiwa amesema changamoto kubwa waliyonayo mwaka huu ni hasara ya Sh. 6.68 milioni iliyotokana na baadhi ya watumishi kugundulika kuwa na vyeti feki, hali iliyopelekea kukosa sifa ya kuwa wanachama wakiwa tayari wamechukua mikopo.