Na Mwandishi wetu
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imetoa agizo kwa Shirika la Madini la Taifa (Stamico) kufuatilia kiasi cha Sh. 1.6 bilioni, fedha ambazo kampuni ya madini ya Acacia inatakiwa kulipa kwa ajili ya mfuko wa hifadhi, lakini hazijulikani zilipo. Mwenyekiti wa kikao cha kamati hiyo Japhet Asunga ametoa tamko hilo baada ya kufanya mazungumzo na shirika hilo kuhusu ripoti ya Mthibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Asenga amelitaka shirika hilo kufuatilia fedha hizo haraka iwezekanavyo na kama fedha zimelipwa basi vielelezo vyake viwasilishwe kwani kamati ya bunge haijafurahishwa na namna matayarisho ya taarifa ya kifedha yanavyoendeshwa katika shirika hilo. Hali ya sasa imepelekea kamati ya bunge kutaka Stamico kutayarisha taarifa za kifedha kwa kufuata kanuni na miongozo ya kimataifa kwa kujumlisha mahesabu yake na kampuni tanzu waliyonayo.
Kampuni ya Madini ya Acacia wamedai kulipa kiasi cha dola za kimarekani 746,336.94 kwenye mfuko wa hifadhi lakini mpaka sasa fedha hizo hazijulikani zilipo.