Bila shaka kwa wengi neno Vicoba sio neno jipya. Limekuwa linatumika kwa muda mrefu katika sehemu mbalimbali ndani ya jamii zetu. Kwa kirefu Vicoba inafahamika kama ‘Village Community Bank’ ikiwa ni kikundi cha watu kati ya 15 hadi 30 wanaofahamiana na kukubaliana katika malengo na katiba, ambao hukutana katika muda uliopangwa ili kupata huduma ya mafunzo ya ujasiriamali na huduma ya fedha. Hapo chini ni baadhi ya sababu za kujiunga na makundi haya.
Vicoba imekuwa kama darasa huru kwa watanzania wengi. Uwepo wa vikundi hivi umesaidia wananchi kujiamini, kujitambua na kuelewa uwezo walionao, hivyo kutumia uwezo huo katika kujiingizia kipato. Kupitia Vicoba watu wengi wamefanikiwa kuondokana na umaskini kwa kupata mafunzo mbalimbali hivyo kutumia fursa hiyo kujikomboa na kutumia uwezo walionao kujiingizia kipato.
Shughuli za ujasiriamali pia zimeendelea kukua kwa kasi kwa kupitia Vicoba. Makundi haya ya watu yamesaidia kuibua mamia ya wajasiriamali wapya na hivyo yamekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi na ukuaji wetu wa uchumi. Kujiunga na Vicoba kunampa fursa mjasiriamali kukutana na wazoefu zaidi ambao wanaweza kuwa washauri na waalimu kwake hivyo kupelekea ujuzi wake kuongezeka. Vicoba pia ni nafasi nzuri ya wajasiriamali kutafuta soko kwa ajili ya bidhaa au huduma wanazotoa.
Aidha kwa kujiunga na Vicoba unapata fursa ya kukutana na watu mbalimbali kutoka serikalini, sekta binafsi, wabia wa vicoba wakati wa mafunzo, mikutano, semina, makongamano, uzinduzi na sherehe mbalimbali hivyo ni nafasi nzuri ya kubadilishana ujuzi, mbinu na uzoefu katika shughuli za kifedha, kiuchumi, kijamii na mfumo mzima wa maisha ya kila siku na maendeleo endelevu ndani na nje ya nchi. Unapata nafasi nzuri ya kujenga mahusiano ya kibiashara na watu mbalimbali ndani ya muda mfupi. Kupata nafasi ya kuona wengine wanachokifanya pia bila shaka kutakuhamasisha na wewe kufanya kazi kwa bidii ili kufikia malengo uliyojiwekea.
Kupitia Vicoba mwanachama anakuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kupata mikopo yenye masharti nafuu. Sote tunajua kuwa taasisi na mashirika mbalimbali hayatoi mikopo kwa urahisi lakini kwa kuwa mwanachama wa Vicoba, unaweza kupatiwa mikopo kwa urahisi zaidi hivyo kufanikisha shughuli mbalimbali za kimaendeleo ambayo ingeweza kukwama bila ya mikopo hiyo..
Taasisi na mashirika mbalimbali kutoka ndani na hata nje ya nje yanafikia Vicoba kwa urahisi ukilinganisha na watu ambao hawajajiunga na makundi haya. Taasisi hizi hutoa misaada kwa Vicoba kwa wingi zaidi kwani inakuwa rahisi kwa wao kuona kile wanachofanya na pia jinsi gani wanaweza kuwasaidia. Tofauti na yule ambaye hajajiunga na vikundi hivi, mashirika yanayoweza kumfikia yanakuwa machache hivyo hupelekea kutumia muda mrefu kutafuta msaada.
Mfumo huu umekuwa na mafanikio makubwa katika kupunguza umaskini kwenye maeneo mbalimbali ambayo tayari unafanya kazi. Ushirikishwaji katika kuanzisha na hata kusimamia vikundi hivi umezidi kuwavutia wananchi wengi. Hivyo basi elimu zaidi kuhusu umuhimu wa vikundi hivi itolewe kwa wananchi hapa nchini.