Imekuwa desturi katika baadhi ya familia kuwa mmoja wao akifanikiwa kimaisha, basi wote wamefanikiwa. Huyo aliyebahatika ndiye atakayewalisha na kuwavisha huku wao wakiwa hawana tena jitihada za kujikomboa. Ni kweli kuwa katika hali fulani unayejiweza kifedha ndio unalazimika kuwasaidia wengine. Ikitokea kuna watoto, wagonjwa,au wazee wa zaidi ya miaka 65 ni jukumu lako kuwatunza. Lakini hali imekuwa tofauti katika jamii yetu ambapo vijana wamekuwa na jukumu kubwa la kutunza ndugu na familia japokuwa ndio kwanza wanaanza maisha yao.
Kuwabebesha vijana mzigo mkubwa kama huo ni kuwarudisha nyuma kimaendeleo. Jifikirie, kama wazazi wanakutegemea wewe kulipa gharama kama chakula, umeme, maji na wakati mwingine hata ada za shule za ndugu zako unapata wapi nafasi ya kutunza akiba na kuwa na mipango ya baadae? Ni kweli kuwa wazazi wetu wamewekeza kwa kiasi kikubwa kwenye elimu yetu ili sisi tuje kuwasaidia huko mbeleni lakini hilo linawapa nguvu ya kuziba mipango yako binafsi? Ni sawa kwa vijana kutafuta hela kwa jasho ili tu kulipa gharama za wengine?
Wapo wazazi ambao baada ya vijana wao kuajiriwa au kujiajiri, wanakuwepo kwa ajili ya kuwapa ushauri kuhusu namna ya kutumia kile ambacho wanaingiza ile wafaidike. Fikiria fursa ambazo vijana hawa wanazipata. Wanajengewa uhuru wa kufanya maamuzi kuhusu namna wanazoweza kutumia kipato chao kuwekeza katika miradi mingine ya maendeleo ambayo huenda itawaingizia fedha zaidi. Lakini wengine hawana bahati hiyo kwani familia inawategemea wao kwa kila kitu.
Nyakati zinatofautiana na kadri siku zinavyozidi kwenda hali ya maisha nayo inazidi kuwa ngumu. Vijana wakiwa katika mazingira haya wanapata wakati mgumu kujiendeleza na kujitegemea. Kijana ambaye ndo kwanza anapiga hatua hii hapaswi kuona kama ndugu zake wenyewe wanamrudisha nyuma. Hii ni sababu mojawapo ya migogoro ndani ya jamii. Wazazi wasione vijana wao ambao bado ni wachanga katika soko la ajira kama njia rahisi ya kupata fedha. Wanatakiwa kuwa mstari wa mbele kuwasaidia watoto wao na bila shaka watoto nao watajipanga vizuri na kuwasaidia huku bado wakiwa huru kufanya miradi yao mingine.
Tujenge mazoea ya kusimama wenyewe bila kutegemea wengine katika maisha. Kila mmoja wetu anafanya kazi kwa bidii ili kupambana na ugumu wa maisha hivyo kuwapa vijana majukumu mazito kunawakwamisha kwa kiasi kikubwa kufanya mambo mengine ya msingi na manufaa zaidi. Tufahamu tofauti ya kuomba msaada pale ambapo unakwama na kumtegemea mtu kwa kila kitu. Kama unakwama, omba msaada na kama haujafanikiwa kupata ajira usikae tu kumtegemea ndugu yako, muombe atumie nafasi yake ili kukusaidia wewe kujiendeleza. Jiongeze usikae tu unategemea vitu vya kupewa.