Teknolojia imeendelea kuwa na manufaa makubwa katika nyanja nyingi za kijamii, tasnia ya biashara ni moja wapo. Ni dhahiri kuwa watu wamekuwa wakiendelea kupata mafanikio zaidi kutokana na matumizi ya teknolojia sahihi katika michakato inayowaingizia kipato. Katika upande wa biashara ndogo hasa zile zinazoanza ni muhimu kuelewa maana ya maendeleo yanayotokana na teknolojia na kuanza kuwekeza katika teknolojia tokea mwanzo ili kuweza kurahisisha ukuaji wa biashara ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wateja lengwa wanafikiwa na bidhaa au huduma husika kwa uharaka zaidi.
Hivyo basi hizi ni faida za matumizi ya teknolojia zilizoboreshwa katika biashara:
- Matumizi ya teknolojia za kisasa hupelekea biashara kujulikana na watu wengi zaidi kwa muda mfupi. Ingawa inashauriwa kutopuuzia njia za kutafuta masoko za kitamaduni kulingana na bidhaa au huduma unayouza pamoja na wateja, lakini teknolojia imekuwa ni muhimu kwa watu wengi duniani kwaajili ya matumizi mbalimbali. Hivyo moja ya njia za kukuza biashara ni kutumia fursa zilizopo katika zama za kidijitali kwamfano kwa sasa kupitia mtandao wa kidijitali wa ‘Instagram’ wafanyabiashara wana uwezo wa kutangaza biashara zao katika mfumo wa ‘Sponsored’ kwa watumaji wote wa mtandao huo dunia nzima.
- Maboresho ya teknolojia yamerahisisha mawasiliano baina ya wateja na mfanyabiashara kwa asilimia kubwa sana, hususani katika mitandao ya kijamii ambapo imekuwa ni rahisi kwa wateja kuchagua bidhaa na kuweza kuzipata bila kufika katika duka au eneo la biashara, pia imekuwa ni rahisi kutoa mrejesho na kuwahamasisha wateja wengine kuweza kununua bidhaa husika, pia imewasaidia wafanyabiashara wengi kurekebisha mifumo yao na utendaji wa biashara zao ili kuweza kuwavutia wateja. Ndio maana kila mfanyabiashara hasa anayeanza anashauriwa kutumia ipasavyo mitandao hiyo tokea awali ili kuweza kupata wateja kwa urahisi, kujifunza na kuweza kujenga utamaduni ambao utawafanya wateja waweze kutofautisha biashara hiyo na nyingine.
- Usimamizi wa hali ya juu wa miradi, ni moja ya faida zinazokuja na maboresho ya teknolojia katika biashara. Ambapo kuna programu mbalimbali za usimamizi wa miradi kwamfano programu za mapato na matumizi, programu za udhibiti wa wafanyakazi nk ambazo kwa pamoja zimekuwa zikiwasaidia wafanyabiashara kujua mtiririko wa fedha katika biashara.
- Suala la usalama ni suala nyeti katika kampuni nyingi. Biashara ndogo na kubwa zinatakiwa kuwa makini katika upande wa usalama ili kuweza kuhakikisha mambo yanakwenda sawa katika kilaupande. Ni muhimu kuliwekea kipaumbele lakini ni vyema kufanya hivyo kulingana na bajeti iliyopo katika biashara. Masuala kama bima, programu za kuhifadhi data, na mambo mengine yanapatikana katika mtandao wa intaneti, jambo la msingi ni kuwa makini na matapeli wa mtandaoni. Hivyo ni vyema kuuliza kwa wafanyabiashara wengine njia wanazotumia kulinda biashara zao kisha chagua zile zitakazofaa biashara yako.
- urahisi wa kufanya malipo unaotokana na teknolojia umeendelea kuwahamasisha wateja wengi kununua bidhaa au huduma pindi wanapozifahamu. Leo hii mbali na mazoea ya kulipa kwa kutumia Kadi za mikopo, Mpesa, Tigopesa, halopesa, Paypal nk, tayari kuna biashara duniani zimeanza kukubali wateja walipie bidhaa katika mfumo wa sarafu za kidijiti kama Bitcoin. Hivyo ni muhimu hata kwa biashara ndogo kuzitumia fursa mpya za malipo ili kuweza kuuza bidhaa katika mifumo mbalimbali ambayo inaendelea kuanzishwa duniani kutokana na maboresho ya teknolojia.
Aidha, kila mfanyabiashara, mdogo au mkubwa ana jukumu la kujua mabadiliko ambayo yanaendelea kufanyika duniani ili kuweza kwenda sawa na mahitaji ya wateja. Hii itasaidia kuimarisha bidhaa au huduma na kutengeneza utamaduni wa kipekee ambao utakutofautisha na washindani wako huku ukiwavutia wateja wengi zaidi ulimwenguni. Elimu ni muhimu, na maamuzi ya kuleta mapinduzi katika biashara yako hayana muda muafaka, anza sasa ili uweze kufikia malengo.