Home HABARI ZA AFRIKA MASHARIKIUJASIRIAMALI Kanuni 5 za ujasiriamali

Kanuni 5 za ujasiriamali

0 comments 322 views

Ujasiriamali umekuwa kimbilio la watu wengi hususani vijana miaka ya hivi karibuni na wengi wao wamefanikiwa kuendesha maisha yao. Japokuwa suala ya kuanzisha biashara linaonekana rahisi, ukweli ni kwamba kuna changamoto mbalimbali ambazo bila kujipanga, zinaweza kukukwamisha kutimiza malengo yako. Sio kila mtu anaweza kuwa mjasiriamali lakini hii haimaanishi kuwa ni watu wa aina fulani tu ndio wanatakiwa kuwa wajasiriamali.

Hizi hapa ni kanuni tano (5) za kuwa mjasiriamali mwenye mafanikio.

Fahamu soko lako:  Ili kupata mafanikio katika biashara yoyote, ni lazima kuwe na wateja wa uhakika ambao watakuwezesha kuingiza kipato. Kabla ya kuingia rasmi katika sekta ya ujasiriamali, ni muhimu kutathmini soko lako na mahitaji yao ili uweze kuwahudumia kulingana na yale wanayohitaji. Huwezi kufika mbali ikiwa biashara itakosa wateja hivyo ni vyema kufanya utafiti wa kutosha ni kujua soko lako vizuri. Kama mjasiriamali, njia mojawapo ya kuongeza mauzo ni kulifahamu soko vizuri na kuhakikisha kuwa huduma au bidhaa inayotolewa inakidhi mahitaji.

Tatua changamoto zilizopo:  Pamoja na kutengeneza fedha, mjasiriamali mzuri anatakiwa kuwa na uwezo wa kutatua changamoto zilizopo katika jamii yake. Ni muhimu kuwekeza katika kutatua matatizo yanayowakabili watu wanaokuzunguka ambao ndio wateja wako wakubwa kwani unapofanya hivyo, una uhakika wa kuingiza kipato. Kwa mfano kama kuna tatizo la upatikanaji wa maji safi, ikiwa wewe utaleta maji katika eneo hilo ni wazi kuwa watu watahitaji huduma yako.

Fahamu wateja wako:  Kama mjasiriamali, unatakiwa kuwafahamu vizuri wateja wako ili kufahamu wanataka nini. Ni muhimu kusikiliza maoni na ushauri wao na wakati huo huo, hakikisha unatimiza mahitaji yao. Ni muhimu kutumia lugha nzuri kwa wateja na kuwafanya wajisikie wanathaminiwa. Unapotengeneza ukaribu na wateja wako, inakuwa rahisi kujua ni vitu gani unatakiwa kuboresha ili kuwapa huduma bora. Kumbuka kuwa kama hakuna wateja basi hakuna biashara.

Kuwa na maono:  Hakuna ujasiriamali bila maono, vitu hivi viwili vinaenda sambamba. Kuwa mjasiriamali bila maono ni sawa na kuendesha gari bila kuwa na sehemu rasmi ya kwenda. Maono yako yatakuongoza kufanya maamuzi sahihi. Jiulize kuwa unataka kuwa nani, lini na unataka kufanya nini baadae? Maono ni kuona kile ambacho watu wengine hawaoni. Ni lazima kuwa na malengo na kufanya jitihada kubwa kuyafikia.

Matumizi mazuri ya fedha:  Unapokuwa makini na matumizi yako ya fedha, unakuwa na nafasi nzuri ya kukuza biashara yako una uhakika kuwa kiasi ulichonacho kinatumika katika kuboresha biashara na sio vitu vingine. Ni rahisi sana kushawishika kutumia fedha katika mambo mengine lakini inashauriwa kutengenisha matumizi binafsi na yale ya biashara ili kuweza kujua maendeleo yako. Kuna programu mbalimbali ambazo unaweza kutumia kuweka kumbukumbu zako za fedha ili kuwa na picha halisi ya muelekeo wako. Ikiwezekana, unaweza kumuajiri mtu ambaye anafahamu vizuri masuala ya usimamizi wa fedha.

Kama unafikiria kuwa mjasiriamali, hakikisha unazingatia kanuni hizi katika mradi wako ili kuwa katika nafasi nzuri za kufanikiwa mbeleni. Ni muhimu kuwa na mpango ambao utakuongoza. Vilevile, jifunze kutoka kwa wajasiriamali wengine ambao wamekuwepo kwa muda muda mrefu zaidi na usisite kuomba ushauri pale unapokwama.

 

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter

Subscribe my Newsletter for new blog posts, tips & new photos. Let's stay updated!