Na Mwandishi wetu
Wadau mbalimbali wa kilimo na viwanda mkoani Kilimanjaro wameomba serikali kuangalia uwezekano ili waweze kuwa na kikosi kazi maalum kwa ajili ya kushughulikia changamoto ya migogoro ya ardhi na maji baina ya wananchi na wawekezaji.
Akizungumzia juu ya suala hilo, Ofisa Mtendaji Mkuu na Utawala wa Kiwanda cha Sukari cha TPC Jaffary Ally amesema mivutano ambayo imekuwa ikijitokeza mara kwa mara kati ya wakazi wa mkoa huo na wawekezaji inapaswa kutafutiwa suluhisho kama serikali imedhamiria kuweka mazingira mazuri kwa ajili ya shughuli za kibiashara.
Jaffary pia ameshauri kuchimbwa kwa visima virefu na kuacha kutegemea maji ya mtiririko pekee ili kumaliza au kupunguza mivutano kuhusu matumizi ya maji baina ya wakulima na wawekezaji katika sekta ya viwanda na kilimo. Ameongeza kuwa kuundwa kwa kikosi kazi kitakachokuja na ufumbuzi wa kudumu kutapunguza adha kama hizi kwa kiasi kikubwa.
Mbali na hayo wawekezaji pia wanakumbwa na changamoto ya hati za uhamiaji na ajira kwa wafanyakazi wanaokuja hapa nchini pamoja na ile ya hati za uhamiaji na vibali vya kufanya biashara kwa wageni.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Anna Mghwira amesema baada ya kukutana na wafanyabiashara wa mkoa huo ili kujadili changamoto pamoja na fursa walizonazo, ofisi yake inaangalia namna ya kuboresha baadhi ya maeneo katika sekta ya biashara.