Rais wa Tanzania, Dk. John Magufuli ameitaka Wizara ya kilimo kufuatilia wamiliki binafsi wa viwanda vya korosho ambao hadi sasa bado hawajaviendeleza Rais Magufuli ametoa maagizo hiyo wakati akizindua kituo cha afya cha Mbonde wilayani Masasi mkoani Mtwara na kuongeza kuwa, wakulima wamekuwa wakizalisha korosho kwa wingi na kupata wakati mgumu wakipeleka bidhaa hiyo sokoni kutokana na viwanda vya ubanguaji kutoendelezwa.
“Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda ubaki huku huku mpaka ukashughulikie viwanda vyote”. Ameagiza Rais Magufuli.
Kuhusu miradi ya afya, Rais Magufuli ameeleza kuwa hadi sasa bajeti imeongezeka kutoka Bilioni 31 hadi Bilioni 270 za kitanzania, ajira 11,152 katika sekta hiyo pamoja na nyumba za watumishi 346. Amewaambia wananchi kuwa hivi sasa wagonjwa kutoka nje ya nchi wamekuwa wakija kutibiwa Muhimbili kutokana na uwepo wa huduma bora. Amewataka wananchi kuwa wazalendo na kutunza mali za umma.
“Nimekuja kufungua (kituo cha afya) kwa niaba ya vituo vingine 352 kwa sababu nilikuwa ninasita kufungua vituo hivi ili nijue ukweli nisije nikafungua vituo hewa”. Amesema