Mwenyekiti wa Shirikisho la wenye viwanda Tanzania (CTI) Dk. Samuel Nyantahe ametoa wito kwa serikali kuwezesha mazingira ya ushindani wa biashara kwa kukamilisha utekelezaji wa sera ya maendeleo kwa sekta binafsi. Dk. Nyantahe amesema hayo katika mkutani mkuu wa 25 wa mwaka na ameongeza kuwa, sera hiyo na sheria zake zina umuhimu mkubwa ikiwa serikali ina malengo ya kufikia uchumi wa viwanda.
Mbali na sera hiyo, Dk. Nyantahe amezungumzia changamoto ya uwepo wa bidhaa feki na namna biashara hiyo inavyoathiri viwanda vya ndani ambapo amesisitiza hatua stahiki zichukuliwe ili kutatua tatizo hilo.
“Viwanda vya ndani vinaathiriwa na bidhaa za magendo na feki kwa kuwa kuna njia nyingi za panya zinapitisha bidhaa. Hili likidhibitiwa itatusaidia kufanya vizuri katika viwanda vyetu”. Ameeleza Mwenyekiti huyo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) Godfrey Simbeye amesema baadhi ya mambo yanayoendelea yanafanya serikali ipate wakati mgumu kuamini sekta binafsi. Simbeye pia ameweka wazi kuwa TPSF inapanga mkakati wa kuweka maadili ya kuendesha biashara na hatua zitachukuliwa kwa wale watakaokiuka taratibu hizo.