Shirika la ndege Tanzania (ATCL) limesaini makubaliano na kampuni ya Hahn Air ya nchini Ujerumani ili kuuza tiketi kupitia mfumo wa mtandao wa kimataifa. Akizungumza kuhusu makubaliano hayo, Mkurugenzi Mkuu wa ATCL Ladislaus Matindi amesema wamefikia maamuzi hayo ili kuwezesha shirika kufanya shughuli zake kimataifa kutokana na ukuaji wa huduma.
Ameeleza kuwa makubaliano hayo yamepitiwa kwa umakini na wanasheria wa serikali hivyo hakutakuwa na madhara yoyote kwa pande zote mbili. Mbali na hayo pia amefafanua kuwa mkataba huo unawaruhusu kutoka muda wowote bila kipingamizi.
Akizungumzia kuhusu makubaliano hayo, Makamu wa Rais wa Hahn Air Steve Knackstedt amesema hii ni taswira mpya inayoashiria ukuaji wa ATCL kwani kampuni yao inatoa huduma katika nchi mbalimbali kote duniani.