Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe amesema kukamilika mapema kwa ujenzi wa barabara za lami pamoja na madaraja ya kisasa mkoani Ruvuma kutaunganisha kwa urahisi mikoa ya nyanda za juu kusini na nchi jirani, hali itakayochochea ukuaji wa uchumi. Mhandisi Kamwelwe amesema hayo wakati akikagua ujenzi wa barabara ya Mbinga-Mbamba Bay KM 60 na kumuagiza Mkandarasi China Henan International Cooperation Group Co. Ltd (CHICO) kukamilisha mradi kwa wakati.
Waziri huyo ameongeza kuwa mkoa huo una fursa mbalimbali za kilimo, uvuvi, usafirishaji na uchukuzi wa mazao na makaa ya mawe hivyo barabara za lami zitakuwa mkombozi kwa wananchi wa mkoa huo.
“Viwanda vingi sasa vinatumia makaa ya mawe tena kwa kiwango kikubwa hivyo tunahakikisha usafiri katika mkoa huu unakuwa wa uhakika ili kuufungua na kuunganisha na mikoa mingine kwa njia fupi na hivyo kuongeza biashara ya ndani kuvutia biashara na nchi za jirani”. Amesema Mhandisi Kamwelwe.
Vilevile, Waziri huyo ametoa wito kwa wakazi wa wilaya za Mbinga na Nyasa kufanya kazi kwa bidii na kuchangamkia fursa za ujenzi wa barabara za lami, uwepo wa makaa ya mawe na uvuvi wa kisasa ili ziwaletee maendeleo.