Kasi ya ujenzi wa mradi wa maghala na vihenge vya kisasa unaofanyika katika wilaya za Dodoma, Songea, Makambako, Mpanda, Mbozi, Sumbawanga, Mbozi, Shinyanga na Babati imeelezwa kumfurahisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Mathew Mtigumwe. Katibu huyo ametoa pongezi kwa uongozi wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) baada ya kutembelea mradi huo katika kanda ya manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.
Mradi wa ujenzi huo ni matokeo ya serikali ya Tanzania na ile ya Poland kutia saini mkataba wa mkopo wa Sh. 124 bilioni (sawa na Dola za Marekani milioni 55) wa masharti nafuu kwa lengo la kuongeza hifadhi ya chakula. Aidha, Wizara ya Kilimo inatekeleza ujenzi huo wa maghala na vihenge vya kisasa ili kuongeza uwezo wa kuhifadhi mahindi kutoka tani 251,000 hadi tani 700,000 kufikia mwaka 2025.
Katibu huyo pia ameeleza kuwa, atawasiliana na Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) ili kuwawezesha wahandisi vijana kushiriki katika mradi huo na kubaki na utaalamu kutokana na teknolojia ya ujenzi huo kuwa ngeni nchini.