Home VIWANDAMIUNDOMBINU Waziri atoa siku 7 mabasi kushusha na kupakia stendi ya Magufuli

Waziri atoa siku 7 mabasi kushusha na kupakia stendi ya Magufuli

0 comment 118 views

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Innocent Bashungwa ametoa siku saba kwa mabasi yote kushusha na kupakia abiria ndani ya Kituo kikuu cha Mabasi cha Magufuli jijini Dar es salaam.

Bashungwa ametoa maelekezo hayo mei 30, 2022 na kumtaka Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Amos Makalla kukutana na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Aridhini (LATRA), wadau na wamiliki wa mabasi kuweka uratibu mzuri wa kusimamia maelekezo ya serikali.

Waziri Bashungwa, ametoa maelekezo hayo wakati akikagua mradi wa Kituo Kikuu cha Mabasi cha Magufuli “Magufuli Bus Terminal” kilichopo wilaya ya Ubungo.

Amesema serikali imetumia kiasi cha shilingi bilioni 50 kujenga kituo hicho hivyo haitakubaliana na watu ambao hawazingatii utaratibu uliowekwa.

“Ninafahamu kuwa Mkuu wa Mkoa, Amos Makalla ameshapokea changamoto ya mabasi kutoingia ndani ya kituo hiki cha Magufuli na mimi nimekuta changamoto bado iko pale pale, sasa kwa sababu ameshanza kulifanyia kazi nampa siku saba awe amekutana na LATRA pamoja na wadu wa mabasi (TABOA) kuangalia utaratibu wa mabasi yote kuingia ndani ya kituo kushusha na kupakia abiria” amesema Bashungwa.

Bashugwa ametoa siku kumi na nne kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ubungo, Kamati ya fedha na uongozi wa kituo cha mabasi cha Magufuli kufanya mapitio na kupeleka mapendekezo ya changamoto ya wapangaji katika kituo hicho ya kulalamikia kiwango kikubwa cha kodi ya pango ambapo wameeleza kwa sasa kiwango cha pango ni shilingi 40,000 kwa mita moja ya mraba.

Aidha, ameagiza kuondolewa kwa magari yote mabovu yaliyoegeshwa kwa muda mrefu ndani ya kituo hicho ambayo ni zaidi ya 40 yanayosababisha ufinyu wa eneo ili kutoa nafasi kwa magari mengine kupata maegesho ndani ya kituo.

Pia amemuagiza Mkuu wa Wilaya Ubungo, Kheri James kuweka utaratibu wa kukutana mara kwa mara na wadau wa kituo hicho na mawakala ili kusikiza na kuweka utaratibu wa kutatua changamoto ambazo zimekuwa zikijitokeza na kuzifanyia kazi kwa ushirikiano.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter