Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Charles Mwijage ametoa onyo kwa wafanyabiashara wanaohujumu viwanda vya ndani vya sukari kwa kuingiza kimagendo sukari kutoka nje ya nchi wakati huo huo akiwahakikishia wawekezaji wa viwanda kuwa, serikali itawalinda. Mwijage amesema hayo bungeni Dodoma wakati akijibu swali la Balozi Dk. Diodorus Kamala, Mbunge wa Nkenge kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) aliyehoji kuhusu kurundikana kwa sukari ikiwa ni matokeo ya wafanyabiashara kuingiza sukari kutoka nje kimagendo.
“Kikosi maalum cha serikali kinafuatilia, naomba nisiende zaidi kwa kuwa kinachofanyika kuna jinai ndani yake na vyombo vya dola vinafuatilia. Wawekezaji wote wa viwanda vyetu serikali inawafuatilia na itawalinda na wale wanaochezea viwanda vyetu uchunguzi ukikamilika hatua kali zitachukuliwa”. Amesema Mwijage.
Waziri Mwijage ametaja baadhi ya taasisi zinazohusika katika kuchunguza suala hili kuwa ni pamoja na Mamlaka ya Udhibiti wa Chakula na Dawa (TFDA), Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) pamoja na Tume ya Ushindani (FCC).
“Hili suala lina jinai na anayehusika atakiona cha moto”. Ameonya Mwijage.