Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo amefungia viwanda takribani 15 vya kuchenjua dhahabu wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga kutokana na kubaini aina mpya ya wizi wa madini unapelekea serikali kukosa mapato. Nyongo amefungia viwanda hivyo baada ya ziara yake ya kushtukiza ambapo alifanikiwa kukamata gramu 102.9 za dhahabu ambayo haikuwa kwenye mfumo rasmi.
Naibu Waziri huyo pia amemsimamisha kazi Kaimu Meneja wa madini kwa mkoa maalum wa madini wa Kahama, Abdurahamani Milandu kutokana na kutosimamia kama inavyotakiwa viwanda hivyo, hali ambayo imepelekea wateja kuibiwa na serikali kukosa mapato stahiki.
Mbali na hayo, Naibu Waziri Nyongo pia amegundua kuwepo kwa mizani ambazo hazina udhibitisho kutoka kwa Wakala wa Vipimo wa Serikali (WMA) na zimekuwa zikikosesha mapato wakati Meneja hakutoa taarifa wala kuchukua hatua zozote dhidi ya wamiliki wa viwanda. Naibu huyo pia ametoa onyo kwa watumishi wa ofisi za madini ambao wamekuwa wakiibia wachimbaji katika kupima dhahabu.